04 March 2013

Shahidi 'amkaanga' Mbunge BadwelNa Rehema Mohamed

MENEJA wa Idara ya Mapokezi katika Hoteli ya Peacock, Bw. Casto Crales, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa, yeye ni miongoni mwa watu waliozithibitisha fedha za mtego wa rushwa alizokamatwa nazo Mbunge wa Bahi, mkoani Dodoma, Bw. Omary Badwel, kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU).

Bw. Creles ambaye katika kesi hiyo ni mmoja wa mashahidi wa upande wa mashtaka, aliyasema hayo mbele ya Hakimu Hellen
Liwa wakati akitoa ushahidi wake huku akiongozwa na wakili kutoka TAKUKURU, Bi. Lizzy Kiwia.

Alidai Juni 2,2012 akiwa ofisini kwake, alifuatwa na mmoja wa walizi wa hoteli hiyo, Bw. Amani Mdede ambaye aliongozana
na Ofisa wa taasisi hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Otieno na kumueleza kuwa, kuna mteja wake amekamatwa na rushwa
hivyo anapaswa kwenda kushuhudia.

Aliongeza kuwa, baada ya kufika kwenye eneo la tukio alimkuta mshtakiwa akiwa amekaa kwenye kiti pembeni yake kukiwa na bahasha ya kaki na kulikuwa na maofisa wengine wa taasisi hiyo.

Alisema maofisa hao walimuomba ashiriki kumfanyia ukaguzi mshtakiwa na kumuamuru Bw. Badwel asimame na kutoa vitu
vyote ambavyo alikuwa navyo mfukoni na kutoa fedha sh.
362,500, kadi ya benki na simu ya mkononi.


Alidai kuwa, maofisa hao walimwamuru aangalie bahasha ya
kaki iliyokuwa mezani na baada ya kuifungua, kulikuwa na fedha
sh. milioni moja zinazodaiwa kukamatwa kwa mshtakiwa.

“Maofisa hao walisema, fedha hizo zilikuwa za mtego hivyo wakaomba tuzihakiki kupitia karatasi ya fomu waliyotupa kama
namba zake zinafanana na zilizoandikwa kwenye fomu ,” alisema.

Alisema fedha hizo zilikuwa noti za sh.10,000 na walianza kufanya ulinganishi wa namba zake na zile zilizokuwa kwenye fomu husika  ambapo namba hizo zilikuwa sawa na zilikuwa za mtego. 

Aliongeza kuwa, katika kufanya ulinganishi huo, alishika fomu
hiyo na kuweka alama ya vyema kwa kila namba inayotajwa inayokuwa sawa na noti husika. Kesi hiyo imeahirishwa hadi
Aprili 4 mwaka huukwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.

Katika kesi hiyo, inadaiwa kati ya Mei 30 na Juni 2,2012, kwenye maeneo tofauti ya Dar es Salaam, mshitakiwa alivunja kifungu
cha 15 (1) (a) cha Sheria namba 11 ya Makosa ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.

Ilidaiwa siku ya tukio, mshitakiwa akijua kuwa ni kosa kisheria, alishawishi apewe sh. milioni 8 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, Sipora Liana.

Inadaiwa kuwa, Bw. Badwel aliomba rushwa hiyo ili awashawishi wajumbe wa kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kupitisha hesabu za halmashauri hiyo, mkoani Pwani.

Katika shitaka la pili, inadaiwa Juni 2,2012 katika Hoteli ya Peacock, iliyopo Dar es Salaam, mshtakiwa alipokea rushwa
ya sh. milioni moja kutoka kwa Liana.

Ilielezwa kuwa, lengo la rushwa hiyo lilikuwa kuwashawishi wajumbe wa LAAC kupitisha hesabu za halmashauri hiyo.

No comments:

Post a Comment