11 March 2013

Sekondari yaanzisha jela ya mateso *Inaitwa “Guantanamo”, siri nzito yafichuka


Na Rashid Mkwinda, Mbeya

WALIMU wa Shule ya Sekondari Forest, iliyopo jijini Mbeya, wanadaiwa kutumia moja ya ofisi za walimu kama chumba cha
mateso kilichopewa jina la “Guantanamo”, ambacho hutumiaka
kutoa adhabu kwa wanafunzi wanaoshindwa kutoa hongo ya
sh. 500 hadi 1,000 wanapofanya makosa shuleni hapo.


Inadaiwa kuwa, wanafunzi wanapofanya makosa mbalimbali
na kushindwa kutoa fedha hizo, hupewa adhabu kali ikiwemo
ya kuinamisha vichwa chini miguu juu.

Adhabu hiyo imepewa jina la “Kuibeba Dunia” ambapo madai ya wanafunzi shuleni hapo, yalifikishwa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), mkoani Mbeya.

Kutokana na malalamiko hayo, taasisi hiyo juzi ilituma makachero wake ambao walifika shuleni hapo kukuta wanafunzi wakipewa adhabu za kijeshi katika chumba hicho.

Wakizungumza namna wanavyopewa adhabu hizo, baadhi ya wanafunzi (majina tunayo), walisema kuna walimu wawili
ambao ndio wanaowapa adhabu wanaposhindwa kutoa
fedha hizo pale wanapokutwa na makosa mbalimbali.

Walisema walimu hao huwa na orodha ya wanafunzi wanaofanya makosa siku nzima na kuwaita mmoja mmoja na wale wanaoshindwa kutoa fedha hukabiliwa na adhabu.

“Ukiingizwa katika chumba hicho mbali ya kuinamisha kichwa
chini miguu juu, pia tunapigwa fimbo zisizo na idadi matakoni,” alisema mwanafunzi mmoja anayesoma kidato cha kwanza.

Mwanafunzi mwingine anayesoma kidato cha tatu shuleni hapo, alisema adhabu hiyo ameikuta tangu anajiunga na shule hiyo ambapo mara nyingi wamepeleka malalamiko yao kwa uongozi
wa shule lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

“Hizi adhabu tumeanza kuzizoea, mwanafunzi akichelewa anasubiri kuitwa Guantanamo na ili ajiokoe anatakiwa kuwa na sh. 500 ambazo mwalimu huzikusanya,” alisema na kuongeza kuwa, yeye binafsi alimweleza mzazi wake ambaye aliahidi kufuatilia suala
hilo kwa undani zaidi.

Akizungumzia tukio hilo jana, Kamanda wa TAKUKURU mkoani humo, Bw. Daniel Mtuka, alisema walimu wawili wamekamatwa juzi wakiwa na sh. 64,000 ambazo walikuwa wakizikusanya kwa wanafunzi ili kukwepa adhabu ya kuingizwa Guantanamo.

Kamanda Mtuka aliwataja walimu hao kuwa ni Faustin Robert na Josephat Mwasote ambao waliwafuatilia baada ya kupata taarifa
za kile kinachofanyika shuleni hapo.

Alisema mbali ya walimu hao kulazimisha kupewa hongo, pia huwavua viatu wanafunzi na kudai havifanani na sare za shule
kisha huwaacha watembee pekupeku na baadaye kuwalipisha
faini ya sh. 1.000 na kuwakabidhi viatu vyao.

“Huu ni mradi ambao walimu wamejiwekea, kwa siku moja zaidi
ya theluthi moja ya wanafunzi hufanya makosa, walimu wanaweza kukusanya hadi sh. 150,000 na kuzitia mfukoni.

“Tumemkuta Mwalimu akiwa na karatasi nyingi zenye majina ya wanafunzi pamoja na sh. 64,000, baadhi ya majina yaliwekwa alama ya vyema kuonesha tayari wamelipa fedha,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo aliyefahamika baadaye kwa jina la Sesilia Kakela, pamoja na kuhojiwa na TAKUKURU alikataa kuwaeleza chochote waandishi wa habari na kusema yeye hajui kitu juu ya tukio hilo shuleni hapo.

“Mimi sijui lolote, nimeona watu wamekuja na kuondoka...sina
la kueleza juu ya kinachoendelea shuleni kwangu,” alisema.

No comments:

Post a Comment