11 March 2013

4 mbaroni wakidaiwa kuchochea udini DarRehema Maigala na Leah Daudi

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za uchochozi wa kidini baada ya kunaswa katika msako mkali uliofanyika jiji hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema
lengo la watuhumiwa hao ni kuchochea vurugu ili kuleta
chuki pamoja na ugaguzi wa kidini nchini.

“Tumefanikiwa kuwanasa watu hawa ambao ni wachochezi
katika mambo ya kidini...majina yao ni Kombo Zuberi (32),
mkazi wa Mburahati, Basote Tandala (24), mkazi wa Gongo
la mboto, Mohamed Sharif (33), mkazi wa Tabata Bima na
Salum Mahambi (46), mkazi wa Tunduma,” alisema.

Hata hivyo, Kamanda Kova alisema kati ya watuhumiwa hao, mmoja alikutwa na nyaraka nyingi za aina mbalimbali alizokuwa akisambaza yeye na wenzake jijini Dar es Salaam na mikoani kwa kusudio la kuleta mifarakano ya kidini nchini.

Aliongeza kuwa, nyaraka hizo ni zile zinazochochea chuki na vurugu dhidi ya Serikali na taasisi nyingine ambapo watu hao
na wengine ambao bado wanatafutwa, imebainika wana mtandao
na mawakala katika sehemu mbalimbali nchini.

Alisema upelelezi unaendelea na ukikamilika, jarda la kesi hiyo litapelekwa kwa wakili wa Serikali ambaye atapitia tuhuma hizo
na watuhumiwa kufikishwa mahakamani.

Wakati huo huo, jeshi hilo kwa kushirikiana na benki mbalimbali nchini ikiwemo Benki Kuu (BoT), limewahadharisha wananchi wenye kadi za zinazotumika katika mashine za kutoa fedha ATM, wasitoe namba za siri wala kadi zao kwa mtu yeyote.

“Mtu akifika kwenye mashine za ATM, asiombe msaada kwa mtu mwingine asiyemfahamu ni vyema kuwatumia wafanyakazi wa benki husika si vinginevyo,” alisema.

No comments:

Post a Comment