11 March 2013

RC Moro awabana Ma DC, DED


Na Severin Blasio, Morogoro

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Joel Bendera, ameahidi kuwachukulia hatua za kinidhamu Wakuu wote wa Wilaya na Wakurugenzi mkoani humu ambao watashindwa kusimamia
usafi wa mazingira katika maeneo yao.

Bw. Bendera aliyasema hayo mwishoni mwa wiki kwenye kikao
cha Kamati ya Ushauri mkoani humo ambapo pamoja na mambo mengine, pia aliwataka Wakurugenzi kutumia sheria ndogondogo zilizopo ili kuhifadhi mazingira na upandaji miti kwa wingi.

Aliwataka Wakurugenzi hao kuhakikisha wanatenga maeneo
ya biashara kwa ajili ya wafanyabishara ndogondogo badala ya kuwaacha wakizagaa barabarani hivyo kusababisha uchafuzi
wa mazingira.

Alisema katika nchi zilizoendelea, wapo wafanyabishara wadogo ambao wamefanyiwa utaratibu unaoeleweka wa kufanyia biashara zao katika maeneo maalumu badala ya kuzagaa barabrani kama ilivyo sasa katika baadhi ya maeneo mkoani humo.

“Manispaa ya Morogoro inaongoza kwa wafanyabishara wengi kuzagaa barabarani hivyo kusababisha uchafuzi wa mazingira, nimeunda Kamati ya Usafi ya Mkoa ambayo itapita katika
maeneo mbalimbali ili kubaini chanzo cha tatizo niweze
kuchukua hatu,” alisema Bw. Bendera.


Alisema msimu uliopita, Mkoa huo ulishika nafasi ya tisa katika suala la usafi wa mazingira ambapo hivi sasa umeshuka na kushika nafasi ya 12 hivyo lazima viongozi na wananchi wafanye kazi ya ziada ili uweze kufanya vizuri katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment