11 March 2013

Rasimu ya Katiba Mpya kukamilika Mei-Warioba


Na Grace Ndossa

MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, amesema rasimu ya Katiba Mpya inatarajiwa kukamilika ifikapo Mei mwaka huu.


Jaji Warioba aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya mchakato wa
uchukuaji fomu kwa wananchi ambao watapenda kuwa
wajumbe wa Mabaraza ya Wilaya na vijiji.

Alisema baada ya tume hiyo kukamilisha mchakato wa kuanzaa rasimu hiyo, wajumbe ambao watachaguliwa watapewa mafunzo maalumu kuanzia Aprili mwaka huu na kuanza kazi ya kuipitia
rasimu hiyo Juni 22 hadi Agosti mwaka huu.

“Rasimu hii itakuwa tayari Mei mwaka huu, hivi sasa tume ipo katika mchakato wa kuchambua maoni yaliyotolewa ili kuiandika
rasimu husika ambayo itajadiliwa na mabaraza haya,” alisema.

“Wito wangu haya mabaraza yanapaswa kuipitia rasimu hii kwa umakini mkubwa ili Watanzania waweze kupata Katika Mpya wanayoitaka,” alisema Jaji Warioba.

Hata hivyo, alisema wananchi wanapaswa kuwa wavumilivu  pamoja na kutoa ushirikiano kwa wajumbe wakati wa mikutano maalumu ambayo itafanyika kabla ya kuanza kazi hiyo.

No comments:

Post a Comment