18 March 2013

Rais Kikwete awashukia wanaokejeli Serikali


Na David John

RAIS Jakaya Kikwete, amewataka baadhi ya wananchi kuacha tabia ya kukejeli jitihada zinazofanywa na Serikali na hasa za kuwasogezea huduma za kijamii wananchi wake ,badala yake waunge mkono jitihada hizo.

Kikwete alitoa kauli hiyo Dar es salaam jana wakati wa maadhimisho ya miaka 25 tangu kuazishwa kwa Hospitali ya Hubert Kairuki.Alisema licha ya Serikali kufanya jitihada kubwa za kuwasogeza huduma wananchi wake bado kuna watu wanakejeli  jitihada hizo badala ya kutoa ushirikiano.

Alisema Serikali imekuwa ikijitahidi kuwahakikisha wananchi wake wanapa pata huduma za kijami kwa karibu zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka ya nyuma lakini wengine wamekalia lawama.

"Nataka wananchi mfahamu kwamba huko nyuma kulikuwa na changamoto kubwa ya huduma muhimu za kijamii na zaidi katika upande wa kupata huduma za kiafya, lakini leo hii Serikali imejitahidi kuweka huduma hizo katika kila zahanati,ikiwa na lengo la kuona wananchi wazifikia kwa wakati, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma,"alisema

Akizungumzia huduma inayotolewa katika Hospitali ya Kairuki, Rais Kikwete alisema hospitali hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa taifa,na imekuwa ikitoa huduma zake kwa uhakika,na imekuwa hospitali ya kwaza nchini kuwa na Chuo Kikuu cha Tiba.

"Ukweli Professa Hubert Kairuki atakumbukwa daima na hasa katika maono yake ya kuazisha hospitali hii,ambayo leo hii inafanya kazi kubwa ya kuwahudumia Watanzania wengi," alisema.

Aliongeza kuwa Serikali itaendela kutoa nguvu zake na hasa katika kuhakikisha huduma za afya zinazidi kusogezwa karibu na wananchi na kufikia lengo la kutokomezwa kabisa vifo vya akina mama na watoto ambayo ni changamoto kubwa katika taifa.

Rais Kikwete alisema Serikali inaendelea kujenga uwezo wa
ndani kwa ajili ya kufanya huduma zinazotolewa nchini zinaaminiwa zaidi na ifikie hatua watu waache kwenda nje.

Katika hatua nyingine aliwataka wananchi hasa akina mama wajawazito kujenga tabia ya kwenda kliniki wanapokuwa wajawazito ili kuepuka vifo visivyokuwa vya lazima. Pia alishauri watu wapime afya zao mara kwa mara kwa lengo la kujilinda.

Naye Mkurugenzi  Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt. Asser Mchomvu, alisema mbali na kuwepo kwa mafanikio mengi, lakini hospitali hiyo inachangamoto kubwa ya kukosa eneo la kutosha kwa ajili ya kuweza kupanua huduma,lakini pia upungufu wa vifaa,pamoja na wataalamu wa kutosha.

Katika hafla hiyo Rais Kikwete alizindua huduma mpya ya Tecknohama hospitalini hapo pamoja na kituo cha kushughulikia matizo ya afya ya uzazi wa akina mama. Hospitali hiyo iliazishwa mwaka 1987 na jana imetimiza miaka 25.


No comments:

Post a Comment