19 March 2013

Polisi yawashikilia tisa kwa ujambazi


Na Masau Bwire, Bagamoyo

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia watu tisa wanaodaiwa kuwa majambazi baada ya kupora sh.milioni 7.5 na kuwajeruhi familia kwa kuwakataka kata mapanga.


Akizungumza jana mkoani hapa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,Bw.Ulrich Mateia, alisema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi katika kitongoji cha Buma.

Kamanda Matei aliwataja majambazi hao kuwa ni Mikidadi Ramadhani (30) mkazi wa Mlandizi, Bw. Ramadhani Hamisi (22) mkazi wa Bagamoyo na Bw. Cheka Mohammed (20) mkazi wa Shimo la Punda, Bagamoyo.

Wengine ni George Mathias (50) mkazi wa Gongo la Mboto Dar es Salaam,Julius Mwita (34) mkazi wa Manzese Dar es Salaam,John Nyaumba (50) mkazi wa Mabibo Dar es Salaam,Bi.Siwema Omari (26)mkazi wa Mlandizi na Bi. Anna Elias (25)mkazi wa Kigongoni, Bagamoyo.

Kamanda Matei alisema majambazi hao wakiwa na silaha mbalimbali za jadi saa 7, usiku wa kuamkia juzi walimvamia Bw. Ganzeli Mohammed (30) mfanyabiashara anayeuza bidhaa mbalimbali kwa bei ya jumla na kufanikiwa kuingia ndani ndani ya nyumba yake baada ya kuvunja mlango kutumia jiwe kubwa maarufu kama 'Fatuma'.

Alisema Bw. Ganzeli alipowaona majambazi hao wakiingia ndani ya nyumba yake alikimbia kwa kutumia mlango wa nyuma na kumwacha mke wake Bi.Zaibu Sabu (30) na mdogo wake Bi. Hawa Msafiri (22) walioteswa vibaya na majambazi kwa kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wakiwalazimisha wawape fedha.

Alisema Bi.Hawa alikatwa misuli na mishipa ya visigino miguu yote miwili baada ya kuwa mbishi na kukataa kutoa fedha kwa majambazi hao ambao mara baada ya kumfanyia ukatili huo alikabidhi sh.mil. 7.5 kwa majambazi hao na kumtaka siku nyingine wakija asibishe kutoa fedha.

Baada ya uporaji huo majambazi hao walitoweka na kwenda kujificha porini katika barabara ya Bagamoyo-Mlandizi baadhi waliwaona na kuwajulisha askari wa  Polisi ambao baada ya kufuatilia walifanikiwa kuwakuta wamelala ndani ya nyumba iliyojengwa kwa nyasi tupu na kuwakamata kirahisi.

Kamanda Matei alisema majambazi hao walikutwa na mali walizopora ikiwemo simu tatu za mkononi,tochi tatu,mashati mawili yalikuwa na damu,kofia mbili aina ya mzula wanazozivaa usoni kuficha sura, mapanga mawili yaliyokuwa na damu ambayo yanadaiwa kutumiwa kuwajeruhi wanafamilia hao, nondo na toi la bastola ambayo hutumia kutishia watu wanapovamia.

Alisema uchunguzi wa awali ulibaini majambazi hao wanapokutana na kupanga mikakati ya shughuli zao za ujambazi ni nyumbani kwa Bi.Anna ambaye huwapikia chakula kabla ya kwenda kufanya uvamizi na ujambazi.

Kamanda Matei alisema nyumbani kwa Bi.Anna walikuta nyaya gunia moja zilizodaiwa kuhujumiwa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) wanazozitumia kutengeneza milipuko ya mabomu ambayo hulipua wakati wakivamia watu ili kuwaogofya.

Alisema majambazi hao watafikishwa mahakamani muda wowote uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili utakapokamilika.

No comments:

Post a Comment