19 March 2013
CCM wagawanyika makundi Shinyanga
Na Suleiman Abeid,Shinyanga
SAKATA la kuachishwa uongozi kwa Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga mjini, Charles Shigino limepokelewa kwa mawazo tofauti na wanachama wa CCM mjini hapa huku wengi wakipinga maamuzi hayo na wengine wakiunga
mkono.
Baadhi ya wana CCM waliozungumza na gazeti hili mjini hapa jana asubuhi walielezea kushitushwa kwao na taarifa za kuachishwa uongozi kwa mwenezi huyo wakisema maamuzi hayo yanaweza kuwa na athari kubwa kwa chama chao katika kipindi cha chaguzi zijazo nchini.
Hata hivyo wakati wanachama hao wakielezea kushitushwa na maamuzi hayo (ambayo hata
hivyo utekelezwaji wake utategemea vikao vya ngazi ya juu) baadhi ya wana CCM wameunga mkono kwa madai kuwa mwenezi huyo anaponzwa na kutokuwa na nidhamu japokuwa ni mtendaji mzuri.
Kwa upande wa wanaopinga uamuzi huo walisema halmashauri kuu ya wilaya ilipaswa kutumia busara katika kujadili tuhuma zinazomkabili mwenezi huyo na kabla ya kuchukua hatua za kumwachisha uongozi ni vyema angepewa kwanza onyo na kuelekezwa
njia anazotakiwa kuzifuata.
Wanachama hao wameelezea wasiwasi wao kwamba huenda baadhi ya wajumbe wa halmashauri kuu ya wilaya wanatumika vibaya na baadhi ya watendaji ndani ya serikali ambao wamekuwa wakifuatiliwa kwa ukaribu na Shigino akiwabana kutokana na kushindwa kuwajibika vizuri kwa wananchi.
“Kwa kweli binafsi nimeshitushwa na hii taarifa ya mwenezi wetu kuachishwa uongozi kutokana na kutuhumiwa kwa mambo mbalimbali,lakini uamuzi huu ni mkali sana, kwa kawaida kwanza angeonywa na kuelekezwa cha kufanya, maana huyu bado ni mgeni katika nafasi aliyochaguliwa,”
“Na iwapo sababu za kuachishwa uongozi itakuwa ni kile kinachodaiwa kuwatetea wananchi nje ya utaratibu unaotakiwa na chama chenyewe basi, ni wazi tutakuwa tunajichimbia kaburi sisi wenyewe katika changuzi zijazo wala tusije tukatafuta
mchawi, maana wanaotetewa na Shigino ndiyo hao wapiga kura,” alisema John Slylivester.
Kwa upande wake mmoja wa makada wa CCM katika kata ya Kambarage mjini hapa Peter Peter alisema Halmashauri Kuu ya CCM imekosea kuchukua maamuzi hayo na kwamba kwa mujibu wa taratibu za CCM, mwenezi huyo alipaswa kuonywa kabla ya kuchukuliwa hatua kali.
“Kisiasa huyu bwana yuko sahihi kabisa, hakuna alichokosea, maana yeye ni mwenezi wa chama moja ya kazi yake ni kukutana na makundi mbalimbali ya watu kushawishi na kueneza sera za chama ili kuweza kuwaingiza ndani ya chama, hata Nape ndivyo anavyofanya, anasema kisha serikali inatekeleza, hakuna alichokosea,” alisema Peter.
Mmoja wa wanachama wanaounga mkono (jina tunalo) alisema hatua iliyochukuliwa kwa mwenezi huyo ni hatua sahihi kutokana na kuonesha kwenda
kinyume na wenzake ambapo alidai mara kwa mara alikuwa akipingana na maamuzi yanayotolewa katika vikao.
“Ni kweli huyu ni mchapa kazi,lakini alikuwa anakwenda kwa kasi zaidi hali ambayo CCM wameona wazi huko mbele kasi yake inaweza kuwaletea matatizo, binafsi nafahamu hakuwa na nidhamu, maana moja ya tatizo lake ni kubisha kila jambo bila ya
kuwasikiliza viongozi wenzake,”
“Mambo ya ndani alikuwa akiyatoa nje, hata hili la kwenda kwa wananchi kusikiliza kero zao alipaswa afuate utaratibu, mara nyingi yeye alikuwa akikurupuka anakwenda peke yake na huko huko anatoa maamuzi,” alieleza mwanachama huyo ambaye ni mmoja wa wajumbe wa halmashauri kuu.
Akizungumza na gazeti hili jana kupitia simu yake ya kiganjani, Shigino alisema hakubaliani na uamuzi wa kuachishwa kwake uongozi kwa vile anaamini hana kosa na kwamba mpaka hiyo jana alikuwa hajapewa barua kuelezwa maamuzi hayo na hivyo yeye bado anajihesabu bado ni mwenezi wa wilaya.
“Haya mambo ya kuachishwa kwangu ninayasikia tu, maana siku ya kikao mwenyekiti alinifukuza na kunitaka nitoke nje ya kikao, sikujua wanajadili nini,na nilipotakiwa nirudi ndani ya kikao sikuelezwa chochote na badala yake tuliendelea
na kikao, kama nilikuwa na kosa ningepewa nafasi ya kujieleza,” alisema Shigino.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment