19 March 2013

Kamati yawarejesha walioacha tiba ya VVU



Na Pendo Mtibuche,Dodoma

KAMATI ya afya katika Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na programu ya Tunajali imeanzisha mkakati wa kuwarejesha kwenye tiba watu 5,358  wanaoishi na VVU (WAVIU) ambao walipotea na kuacha huduma hizo mkoani hapa.


Hayo yalielezwa jana na mratibu wa mkakati huo wa  kuwarejesha kwenye tiba watu wote wanaoishi na virusi vya Ukimwi mkoni hapa, Dkt.Zainabu Chaula wakati wa kuzindua mkakati huo ndani ya mkoa wa Dodoma.

Dkt.Chaula alisema kuwa kamati hiyo ya afya mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na programu ya Tunajali imeanzisha mkakati wa kuwarejesha kwenye tiba watu wote ambao wanaishi na VVU na walishasajiliwa kwenye vituo 33 vya huduma na tiba za VVU (Cts) lakini kwa sasa wameacha kutumia huduma hizo.

Alieleza kuwa mradi huo unaendeshwa kwa msaada wa watu wa marekani kupitia shirika la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kama sehemu ya mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na Ukimwi (PEPFAR).

Hata hivyo Dkt.Chaura alisema kuwa tathimini ya  wagonjwa na kuwarejesha kwenye huduma ni muhimu sana katika kuwawezesha kuanza matibabu hivyo  kupunguza uwezekano wa maambukizi mapya ya VVU kwenye jamii.

Kwa upande mwingine alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 2012 Mkoa wa Dodoma ulisajili kwa aili ya huduma za VVU watu 22,238 ikiwa ni asilimia 34 ya watu 66,000 wanaokadiliwa kuwa na maambukizi ya virusi  vya ukimwi mkoani hapa.

Kwa upande mwingine pia alisema kuwa watu 13,800 kati ya hao 22,238 waliosajiliwa wanatumia dawa na hivyo hali zao zinaendelea vizuri na wanaendelea kufanya shughuli zao za kila siku.

Pamoja na mafanikio alieleza kuwa zipo changamoto mbalimbali kubwa ikiwa ni pamoja na  wahusika kutotumia huduma hizo hali ambayo inachangia kudhorota kwa afya zao na hata kupoteza maisha.

“Takwimu zinaonyesha kuwa watu waishio na VVU (WVIU) wapatao 5,358 mkoni hapa hawajulikani walipo kwani hawafiki kwenye vituo vya huduma na tiba kupata huduma .

Kwa upande wake naye Katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma, Bi.Rehema Madenge akizungumza katika uzinduzi huo wa kampeni ya kuwarejesha waliopotea  katika tiba ya VVU alisema kuwa ni kampeni nzuri kwani itasaidia kuondoa fikra za watu kujificha na kuendelea kupata maambukizi mengine mapya.


No comments:

Post a Comment