05 March 2013

Polisi wauawa Uchaguzi Mkuu Kenya


NAIROBI, Kenya

KATIKA hali isiyo ya kawaida, watu wasiopungua 17 wameuawa wakiwemo Maofisa sita wa polisi katika Mkoa wa Pwani, nchini Kenya siku moja kabla ya Uchaguzi Mkuu ulioanza jana.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Aggrey Adoli, amelishutumu kundi linalopigania kujitenga la Mombasa Republican Council (MRC), ambalo siku za nyuma lilitishia kuvuruga uchaguzi huo.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Bw. Raila Odinga na Naibu wake,
Bw. Uhuru Kenyatta, ndio wanaopewa nafasi kubwa ya kushinda miongoni mwa wagombea wanane wa kiti cha urais.

Akizungumza baada ya kupiga kura, Bw. Odinga alisema raia
wa Kenya wataamua kama kweli wanataka mabadiliko ambapo
Bw. Kenyatta alidai yeye ana matumaini ya kushinda na
kuongeza kuwa, ataheshimu matokeo ambayo yatatangazwa.

Kwa mujibu wa Sauti ya Ujerumani (DW), Bw. Kenyatta na mgombea mwenza, Bw. William Ruto ni miongoni mwa watu wanne wanaoshtakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC.

Viongozi hao wanadaiwa kuhusika na vurugu za kikabila
zilizoibuka baada ya Uchaguzi Mkuu 2007, ambapo zaidi
ya watu 1,200 waliuawa.

No comments:

Post a Comment