05 March 2013

Mapya zaidi yabuka kifo cha kigogo UVCCM



Na Pamela Mollel, Arusha

TUKIO la kufariki kwa aliyekuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, mkoani Arusha, Benson Mollel (26), limevuta hisia za wakazi
wa Mkoa huo baada ya vitu mbalimbali kupatikana katika
chumba alichokuwa amelala.


Vitu hivyo ni bastola, kadi za benki, simu na fedha ambazo kiasi chake hakijajulikana ambazo zilikutwa katika chumba hicho
ndani ya Hoteli ya Lush Garden Business iliyopo jijini humo.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Liberatus Sabas, alisema
jeshi hilo bado linaendelea na uchungunzi wa kifo hicho ambapo
mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote.

“Pamoja na kifo hiki kutokea ghafla, tunaendelea kuwasiliana na familia ya marehemu kujua kama watakubali mwili huu ufanyiwe uchunguzi...mbali ya marehemu kujishughulisha na siasa, alikuwa akifanya kazi katika Kampuni ya Madini ya Manga Gems iliyopo jijini Arusha,” alisema Kamanda Sabas.

Marehemu Mollel alifariki juzi ndani ya hoteli hiyo iliyopo Mtaa
wa Jacaranda katika mazingira ya kutatanisha huku mwili wake ukiwa uchi.

Mtumishi wa chumba cha kuhifadhia maiti Katika Hospitali ya Mkoa ya Mt. Meru (jina linahifadhiwa), alithibitisha kuona mipira (kondumu), zilizokuwa zimehifadhiwa katika shuka alilobebewa marehemu wakati mwili wake ulipopelekwa na polisi.

“Tuliupokea mwili huu juzi saa 8:30 mchana ukiwa
umezungushwa kwenye shuka ambazo ndani yake
kulikuwa na mipira miwili ya kiume na moja
ikiwa imetumika,” alisema.

Aliongeza kuwa, muda mfupi baada ya mwili huo kuingizwa mochari polisi walioupeleka walirudi na kuichukua mipira hiyo.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Frida Mokiti, alisema hadi jana walikuwa hatujapata taarifa kutoka Jeshi la Polisi kama wanapaswa kuufanyia uchunguzi mwili huo.

Mwenyekiti wa kamati ya mazishi ambaye ni Diwani wa CCM, Kata ya Mlagngarini, Bw. Mathias Manga alisema taratibu za mazishi pamoja na misa ya kumwombea marehemu zitafanyika kesho nyumbani kwao Kata ya Daraja Mbili.

Alisema hadi sasa, wanamsubiria baba mzazi wa marehemu ambaye yuko jijini Mwanza ambapo mjomba wa marehemu, Bw. Daniel Mollel, alisema familia wameshtushwa na kifo hicho kutokana
na mchango wake.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Dkt. Wilfred Ole Soilel, alisema chama chao kimepokea msiba huo kwa mshtuko mkubwa kwani marehemu alitumia busara kuwaunganisha vijana ndani ya chama hicho.

1 comment:

  1. HIVI HATA HUYU NI SAHIHI KUSEMA MUNGU KATOA NA MUNGU KATWAA JE ALISALIWA KWA TARATIBU ZOTE AU TARATIBU ZILIACHWA

    ReplyDelete