13 March 2013

Abiria reli ya kati Dom wakwama
Na Elizabeth Joseph, Dodoma

MVUA zinazoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko katika maeneo ya Godegode, Miganga na Gulwe, mkoani Dodoma, zimesababisha abiria zaidi ya 1,000 ambao wanatumia reli ya kati, kushindwa kuendelea na safari kutokana na njia za reli kuharibika.


Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakato tofauti jana katika Stesheni ya Reli mkoani hapa, abiria hao waliokuwa wakitokea mkoani Kigoma kwenda Dar es Salaam, wapo eneo hilo tangu
Machi 10 mwaka huu ambapo hivi sasa wameishiwa fedha za
matumizi ya chakula hivyo kupata usumbufu mkubwa.

“Posho ya chakula tuliyopewa kwa siku ni sh. 2,500 ambayo ni ndogo sana, shughuli zetu tulizokuwa tukizifanya Dar es Salaam
pia zimekwama hivyo kutuongezea umaskini,” walisema.

Mmoja kati ya abiria hao, Bw. Hassan Ayubu ambaye ni mwanafunzi, alidai Serikali inapaswa kuliangalia suala hilo kwa
kina kwani abiria wanaingia hasara kubwa kwa sababu ya kuchelewa kufika Dar es Salaam ili kuendelea na shughuli zao.

“Kwa kweli tunapata shida sana kutokana na uharibifu wa njia
ya reli, miongoni mwa abiria ni wagonjwa wanaochelewa kupata matibabu na wafanyabiashara ambao biashaza zao wanazisimamia wenyewe,” alisema Bw. Ayubu.

Naye Bi. Anna Robert, alisema usafiri huo si salama tena kutokana na miundombinu yake kuchakaa hali ambayo inawapa waiswasi abiria juu ya usalama wao pamoja na usumbufu wasioutarajia.

Baadhi ya abiria walilalamikia kunyimwa posho hiyo kwa madai
ya kutokuwa na vitambulisho licha ya kukatiwa tiketi hizo na wafanyakazi wa Shirika la Reli (TRL).

Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo cha Reli ya Kati mkoani hapa, Cracsus Romana, alikiri kuwepo kwa tatizo la uharibifu wa njia ya reli katika eneo la Gulwe, Godegode na kufafanuwa kuwa, mafundi wapo eneo la tukio na abiria walitarajiwa kuondoka jana saa 12 jioni.

“Abiria wote waliokata tiketi kwa kufuata utaratibu tunawapa sh. 2,500 kwa siku kwa ajili ya chakula...tatizo la kuharibika kwa njia
ya reli limetokana na mafuriko yaliyokea,” alisema.

No comments:

Post a Comment