04 March 2013

Moravian: Msemaji wa Kanisa ni M/kiti tuNa Charles Mwakipesile, Mbeya

KANISA la Moravian nchini, Jimbo la Kusini, limemkana Mchungaji Emaus Mwamakula na kusema yeye si msemaji wa kanisa hilo Jimbo la Misheni, kama anavyodai.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya, Mwenyekiti wa kanisa hilo, Mchungaji Clement Mwaitebele, alisema kwa mujibu wa katiba yao, msemaji wa kanisa ni yeye.

Alisema Mchungaji Mwamakula si msemaji wa kanisa hilo pia ni miongoni mwa wachungaji 14 waliofukuzwa hivyo kujivika cheo hicho ni kukiuka katiba na kuudanganya umma.

“Mwenyekiti ndiye msemaji wa kanisa kwa kujibua wa katiba, ibara ya 98, nasikitika anapotokea mtu mwingine na kudai yeye
ndiye msemaji wetu...namtaka aache kulichanganya kanisa la Mungu kwani tayari amefukuzwa uchungaji,” alisema.

Aliongeza kuwa, mgogoro uliokuwepo kati ya wachungaji hao na kanisa tayari umekwisha
na kinachosubiriwa ni kesi ambazo zilizofunguliwa katika mahakama.

Mchungaji Mwaitebele alisema, kesi hizo hazihusiani na hatua ya kufukuzwa wachungaji waliokiuka utaratibu akiwemo Mchungaji Mwamakula anayedai ni msemaji wa kanisa hilo.

“Tunamshukuru Mungu baada ya mgogoro huu kuisha na kazi
ya Mungu inasonga mbele, uongo uliokuwa unaenezwa kuwa
Bodi ya Dunia inakuja kwa ajili ya kuharibu taratibu za kanisa.

“Bodi ya Dunia ilikutana na walengwa na kuwaeleza msimamo
wao na kila Mchungaji wa kanisa hili duniani anafahamu wazi
kuwa, kama atakiuka taratibu na kufukuzwa, si Mchungaji tena
wa kanisa hivyo nashangaa kuona bado hawajaondoka kwenye
nyumba kitendo ambacho hakiwezi kuvumilika,” alisema.

Alisema jimbo hilo linaendesha mambo yake kwa kufuata
misingi ya kisheria na taratibu hivyo hawataki kuona taratibu
zinakiukwa kwa masilahi ya watu wachache kutokana na
maagizo yaliyotolewa na vikao halali.

Mchungaji Mwaitebele alisema, kanisa hilo haliongozwi na mtu mmoja bali linaongozwa na vikao halali hivyo hawezi kutokea mtu mmoja nje ya katiba na kujipachika wadhifa ambao hautajwi eneo lolote kwenye katiba na kuleta vurugu.

Alionya kuwa, kama ukiukwaji wa taratibu za kanisa utaendelea, Halmashauri Kuu haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa mujibu wa katiba ya Kanisa na kusisitiza jimbo lake litaendelea kusimamia eneo la Misheni ya Dar es Salaam.

2 comments:

  1. Ni kweli kabisa, huyu ngugu Mwamakula ni mleta fujo ndani ya kanisa kwani ni Bingwa wa kueneza maneno ya uongo. Mimi nilishangaa kuona kuwa Kanisa letu eti lina katibu wa idara ya mawasiliano kitu ambacho hakimo katika katiba ya kanisa letu. Ni jambo la aibu kwa baadhi ya watu wasomi hasa wa Dar Es Salaam kuendeshwa na utashi wa mtu pasipo kuzingatia katiba. Kwani inashangaza watu anafuata tu pasipo kuhoji hiyo idara ipo kwa misingi ipi? Mch. Mwaitebele, hongera kuwa kupambana na uasi na upotofu huu ndani ya kanisa letu

    ReplyDelete
  2. Nchi inaendeshwa kwa mujibu wa katiba, vivyohivyo mashirika yote yawe ya binafsi au ya Dini yana katiba zilizosajiriwa na serikali kwa mujibu wa katiba hivyo mtu yeyote anaendesha mambo yake kinyume cha taratibu za Nchi, anahatarisha amani ya Nchi yetu. Hivi huyu Mamakula iweje anatanua matamvua wakati hatambulikani kisheria kama msemaji wa kanisa, je kauli zake zikihatarisha amani nani awajibike? kanisa! hivyo ni vema aripotiwe kwenye vyombo husika ili achukuliwe hatua stahili. Watu kama yeye wanaojitwalia madaraka kinyume cha katiba wapo chini ya mkono wa sheria, wana kesi ya kujibu. Msimwache

    ReplyDelete