15 March 2013

Moravian laguswa na shambulizi la Kibanda


Na Mwandishi Wetu

UONGOZI wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT), Jimbo la Kusini, umelaani vikali tukio la kuvamiwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Bw. Absalom Kibanda na kudai vyombo vya Ulinzi na Usalama, vinapaswa kuwafuatilia na kuwakamata watuhumiwa hao.


Mwenyekiti wa jimbo hilo, Mchungaji Clement Mwaitebele, alitoa msimamo huo alipozungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kutoka Dodoma, ambako viongozi makanisa yaliyo chini ya CCT, wanaendelea na vikao vyao vya maamuzi.

Alisema kanisa limepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa
na kuvishauri vyombo hivyo, kufanyia kazi dalili zozote za uovu kwenye makanisa na nyumba nyingine za ibada.

“Kibanda ni Mwenyekiti wa Jukwaa huru la wanahabari nchini lakini unyama aliofanyiwa haustahili kutufanya tubaki kimya kwa sababu zozote,” alisema Mchungaji Mwaitebele.

Aliongeza kuwa, waumini wa kanisa hilo nchini kote wanamtakia Bw. Kibanda matibabu mema ili aweze kupona haraka na kuendelea na wajibu wake katika kipindi hiki ambacho Taifa linabakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii.


“Tumeamua kutenga siku maalumu kwa ajili ya kumuombea maana haya yaliyotokea ni majaribu ambayo msingi wake ni uwajibikaji, lakini tunawatia nguvu na kuwaomba muachieni Mungu Muumba, aweze kujibu kilio chenu,” alisema Mchungaji Mwaitebele.

Wakati huo huo, Mchungaji Mwaitebele, aliwataka Wahariri wa vyombo vya habari nchini, kutomtambua mtu anayejiita Mkuu wa Kitengo cha Habari Jimbo la Misheni ya Mashariki na Zanzibar.

Alisema mara kadhaa, mtu huyo ambaye alikuwa Mchungaji lakini hivi sasa ni mmoja kati ya Wachungaji 14 waliofukuzwa na kanisa, amekuwa akitoa taarifa za kutishia kuwashtaki baadhi ya waandishi wa habari na Wahariri wao.

“Huyu amewahi kumtishia Bw. Kibanda, baada ya mwandishi
wake kuandika habari zilizohusu kikao kilichofanyika Usharika
wa Tabata na Wahariri wa magazeti mengine,” alisema.

Alisema mtu huyo pia amekuwa akiwataka Wahariri kukanusha habari zinazoandikwa na magazeti yao wakati yeye hana mamlaka kisheria kwani msemaji wa kanisa hilo ni Mwenyekiti.

“Kwa mujibu katiba ya kanisa hili, inatamka wazi wazi kuwa Msemaji Mkuu wa mambo yote ya kanisa, serikali, ushirikano
wa makanisa mengine na majimbo mengine ni Mwenyekiti.

No comments:

Post a Comment