15 March 2013

Membe: Sihusiki kumtesa Kibanda *Afananisha jambo hilo na kuchafuliwa kisiasa


Na Rachel  Balama

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, amesema hausiki na hana sababu ya kuhusika
na vitendo vya ukatili na unyama aliofanyiwa Mwenyekiti wa
Jukwaa la Wahariri (TEF), ambaye pia ni Mhariri Mtendaji
Mkuu wa Kampuni ya New habari, Bw. Absalom Kibanda.

Taarifa iliyoitoa Dar es Salaam jana kwa vyombo vya habari, Bw. Membe alisema amesikitishwa, kushangazwa na gazeti moja (si Majira), ambalo lilimuhusisha na uvamizi wa Bw. Kibanda.

Alisema habari hiyo ambayo ilikuwa na kichwa cha habari kinachosema “sakata la kuteswa kwa Kibanda Membe atajwa”, haikuwa na ukweli wowote.

“Binafsi sina nia, genge wala fedha za kufanya ukatili kama huu, katika maisha yangu sijawahi kugombana na Bw. Kibanda na wala hajawahi kunifanyia ubaya wowote na sina uhasama naye,” alisema.

Bw. Membe alisema, taarifa iliyotolewa dhidi yake ni mwendelezo wa mkakati wa kisiasa wa kumchafulia unofanywa na mahasimu wake kwa kuwaondoa Watanzania katika ya kutaka kufahamu ukweli wa jambo hilo.

Aliongeza kuwa, yeye anaamini ukweli kuhusu suala hilo utajulikana na yeyote mwenye ushahidi wa kweli aoneshe uzalendo wake kwa kutoa taarifa katika vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Aliwaomba Watanzania wavute subira na kuviachia vyombo hivyo vifanye kazi yake ili ukweli uweze kubainika na kusisitiza kuwa, anaendelea kushauriana na mwanasheria wake aweze kuchukua hatua kutokana na kuchafuliwa.

2 comments:

  1. tell them next president,waache ushahidi wa kubuni!

    ReplyDelete
  2. ya elias,haujayachomeka yasijulikane

    ReplyDelete