19 March 2013
Moat yaitaka Serikali kutumia analojia, digitali
Na Goodluck Hongo
WAMILIKI wa Vyombo vya Habari Nchini (Moat) wameitaka Serikali kutumia mifumo yote miwili ya analojia na digitali kwa wakati mmoja hadi kufikia mwaka 2015 ambapo itakuwa mwisho wa kutumia analojia.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa Moat Bw.Reginald Mengi alisema wao hawapingi nchi kuingia katika mfumo huo ila wanachotaka ni mifumo yote itumike pamoja ili wananchi wapate haki ya kupata habari.
Alisema wananchi wengi wanakosa haki yao ya kupata habari ambapo ibara ya 18 ya katiba ya nchi yetu inasema kuwa ni haki ya kila mwananchi kupata habari.
"Sisi kama wamiliki wa television hatupingi digitali kwani tumewekeza mamilioni ya dola katika mitambo ya digitali ila tunachokiomba sisi ni kwamba Watanzania hawakujiandaa vya kutosha kutoka analojia kuingia digitali hivyo tuliomba wapewe muda ili wananchi wajiandae, "alisema Bw.Mengi.
Aliongeza kuwa leseni za kujengwa kwa miundombinu ya digitali zilianza kutolewa mwaka 2010 na mchakato wake wa kuingia digitali ulianza mwaka 2006 sasa tangu kutolewa rasmi kwa leseni hizo ni miaka miwili tu imepita ambapo ni muda mdogo ambapo mwisho wa kutumia analojia ni Juni 17, 2015.
Aliongeza kuwa nchi tajiri duniani walichukua miaka mingi kuingia katika mfumo huo wa digitali kutokana na kutojiandaa kumesababisha wananchi wengi kutoangalia taarifa ya habari na badala yake televisheni hizo sasa zinatumika kuangalia mikanda.
"Nchi ya Uingereza ilichukua miaka 14,Marekani miaka 11 na Japani miaka nane kutoka mfumo wa analojia kwenda digitali lakini sisi ni miaka miwili tu na tulijaribu kuzungumza na Serikali lakini hawakutusikiliza, tunakimbilia nini wakati Mauritania ndio nchi pekee Kusini mwa Jangwa la Sahara ambayo imezima mitambo hiyo ya analojia wakati Kenya na Uganda wanatumia mifumo yote miwili, "alisema Bw.Mengi.
Alisema viongozi ni lazima wawatete wananchi ambao kwa sasa ndio waliowachagua lakini wajue kuwa watarudi tena kuwaomba kura ili wachaguliwe viongozi ambapo kama mtu akikosea ni vema akaomba samahani lakini akishindwa basi awajibike kwa kuwa kosa limeshatokea.
Bw.Mengi alifafanua zaidi kuwa makampuni mengine kutoka nchini China yamesamehewa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ili waingize ving'amuzi vingi zaidi lakini makampuni mengine hapa nchini hayakusamehewa kodi na Serikali ya Afrika kusini ilitoa fedha za ruzuku milioni tano kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kumiliki ving'amuzi ili wapate haki yao ya kupata habari.
Naye Mkurugenzi Mtendaji kutoka kampuni ya Sahara media group Bw.Samweli Nyala alisema kwa sasa teknolojia mpya inayotumika katika televisheni ni DVBT2 badala ya DVBT.
Alisema kwa sasa asilimia 75 ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam hawaangalii taarifa ya habari ambapo muda ni mrefu wa kuingia katika digitali na kwanini tuingie mapema?.
"Tanzania ndio nchi ya mwisho kupata televisheni lakini ndio nchi ya kwanza kuzima mitambo ya analojia wakati wenzetu wengine wanakwenda nayo yote miwili ili wananchi wapate haki yao ya kupata taarifa, " alisema Bw.Nyala
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment