Na Casmir Ndambalilo, Newala
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Kapteni mstaafu George Mkuchika, ameiomba Serikali kupitia Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kuongeza muda na kasi ya kusambaza umeme unaotokana na gesi iliyogundulika mkoani Mtwara ili kuchochea
maendeleo ya wananchi.
Bw. Mkuchika ambaye pia ni Mbunge wa Newala, aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Mahakama wakati akihitimisha ziara yake ya siku 10 ili kutoa
elimu inayohusu gesi kwenye kata na vijiji mbalimbali.
Alisema baada ya kutoa elimu hiyo, imesaidia wananchi mkoani humo kukiri upotoshaji uliofanywa na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati juu ya matumizi ya gesi iliyopatikana.
“Mimi mbunge wenu kazi kubwa ambayo nitaifanya ni kuiomba Serikali kupitia TANESCO kuhakikisha kasi na muda uliotolewa
kuwaunganishia umeme wananchi wa Mkoa huu hususan waishio vijijini, unaongezwa ili kila mtu afaidike na nishati hiyi kwa shughuli mbalimbali za maendeleo.
“Pia nitaomba punguzo la gharama za kuunganisha umeme kutoka sh. 500,000 hadi sh. 99,000 liendelee kuanzia Juni mwaka huu hadi kufikia miaka mitano ikiwezekana,” alisema.
Aliongeza kuwa, kwa miaka mingi Mkoa huo umekuwa na tatizo la upatikanaji umeme wa uhakika, jambo ambalo wananchi wengi waliokuwa na uwezo wa kuwekeza katika miradi mbalimbali
ya maendeleo kwa kutegemea nishati hiyo, wameshindwa
kufanya hivyo.
“Baada ya kupatikana gesi, sasa hakuna sababu ya wananchi wa Newala na Mkoa wa Mtwara kushindwa kutumia fursa iliyopo kwa kuanzisha miradi itakayotumia umeme ili kujikwamua na umasikini.
“Suala la kupinga gesi isiende Dar es Salaam ni la kisiasa na wanaoposha ni kwa maslahi yao...Newala, tusipoteze muda wetu kwa ajili ya kupinga gesi isisafirishwe, hivi ninavyozungumza Mkandarasi yuko kazini kutekeleza mradi wa ujenzi wa
bomba hilo,” alisema Bw. Mkuchika.
Alisema jambo la msingi ni kuhakikisha wapotoshaji kama waliojitokeza kwenye suala hilo hawasikilizwi kwani Serikali iliyopo madarakani iko makini na mara zote mipango yake ni kuhakikisha wananchi wake wanafaidika na rasilimali za Taifa.
No comments:
Post a Comment