04 March 2013

'Mfumo wa elimu sasa uangaliwe upya'


Na Raphael Okello, Bunda

MFUMO wa Elimu nchini, bado haujawawezesha wahitimu
kuwa wabunifu na kuwapa maarifa ya kupambana na maadui
watatu ambao ni ujinga, maradhi na umaskini.

Mbunge wa Viti Maalumu CCM, mkoani Mara, Bi. Esther Bulaya, aliyasema hayo hivi karibuni katika mjadala maalumu wa elimu ulioandaliwa na asasi ya kiraia ya Volunteering Network
Foundation (VONEFO).

Alisema ipo haja ya Bunge, kuujadili upya mfumo wa elimu
ambao utasaidia kuwakomboa Watanzania kwani uliopo,
unachangia elimu kutolewa kinadharia zaidi badala ya
vitendo na kusababisha nchi ikose wataalamu wazuri.

“Katika nchi nyingine, elimu inayotolewa huwawezesha raia
wao kuwa wabunifu hivyo kubadili maisha yao, elimu iliyopo
nchini haiangalii ubora wa elimu ya wahitimu,” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu nchini (CWT) wilayani Bunda,
Bw. Francis Ruhumbika, aliitaka Serikali kuboresha masilahi ya walimu na kufanya mazingira ya kufundishia kuwa rafiki.

Mwenyekiti wa VONEFO, Bw. Mongson Kabeho , alisema lengo
la mjadala huo ni kuwawezesha wadau wa elimu nchini kuchambua mfumo uliopo na kutoa mapendekezo kama unakidhi viwango vya ubora wa kutoa ajira na kubadili maisha ya Watanzania.

No comments:

Post a Comment