11 March 2013

Mbatia akataa ujumbe tume ya PindaNa Darlin Said

MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. James
Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa, amesema hakubaliani na uteuzi uliofanywa na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, kuwa mmoja wa wajumbe katika tume ya kuchunguza sababu za kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012.


Alisema tume hiyo ina mgongano wa kimasilahi ambapo
mbali ya kukataa uteuzi huo, hadi sasa hajapata barua rasmi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bw. Mbatia, kutopata barua hiyo kumemfanya ashindwe kufahamu
majukumu ya tume ingawa ameyasikia kwa uchache katika
vyombo mbalimbali vya habari.

Alisema miongoni majukumu ya tume ni kuchunguza mtaala
kama unakidhi mfumo wa elimu nchini na kusisitiza kuwa, tayari alishapeleka hoja binafsi bungeni na kudai haifai.

“Siwezi kuchunguza kitu ambacho sikiafiki, kufanya hivyo
ni sawa na kula matapishi yangu,” alisema Bw. Mbatia na
kuongeza, hata kama atapata taarifa kimaandishi itakuwa
ngumu kushiriki kwa sababu atashindwa kuchambua
matokeo ambayo yatapatikana kwenye tume.

Aliongeza kuwa, haitakuwa jambo jema kwake kama atashiriki katika tume hiyo kwani si njia bora ya kupambana na janga hilo
la Taifa ambapo hadidu rejea za tume hiyo hazitashughulikiwa
kwa upana zaidi

“Kushiriki katika tume hii ni sehemu ndogo sana ya hoja yangu hivyo nitakuwa nimeshiriki dhambi ya kimfumo ya kuvuruga mfumo wa kazi za Bunge...nitakuwa nimehama kutoka benchi
la wabunge na kukalia benchi la Serikali,” alisema.
 
Bw. Mbatia alisema, tangu nchi ipate uhuru haijawahai kuwa na mitaala rasmi ya kufundishia na kuishauri Serikali ni vyema ikarejea katika ripoti ya 2011 inayotokana na uchunguzi wa tatizo hilo yenye majibu yote ambayo tume hiyo inakwenda kuchunguza.

Wakati huo huo, Bw. Mbatia alisema amemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete, kuangalia kwa makini mfumo wa elimu nchini
ili kujua tatizo ni nini.

Alisema ni vyema ikaundwa tume ya kuchunguza mfumo wa elimu kama ilivyokuwa tume ya Makwete ya mwaka 1980-1985, ambayo  iliundwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere iliyokuja na matokeo mazuri katika sekta ya elimu.

Aliongeza kuwa, Rais Kikwete anajitahidi sana kuhakikisha anaboresha mfumo wa elimu kwani ameweza kuomba msaada
kutoka Seikali ya Uholanzi kuchunguza mfumo wa elimu nchini na kufanikiwa kupata dola za marekani milioni 5.7 ila hana wasaidizi wazuri kwani pesa hizo hadi sasa hazijulikani zilipo.

No comments:

Post a Comment