04 March 2013

Mwanafunzi kidato cha nne awaua


Na Mercy James, Njombe

MWANAFUNZI wa kidato cha nne katika Sekondari ya Ikuwo, Tarick Mbwilo (18), ameuawa na watu wasiofahamika pamoja
na mama yake mzazi Ester Mwalukolo (49).

Tukio hilo ambalo limetokea Februari 29 mwaka huu, katika
Kata ya Ikuwo, Wilaaya ya Makete, mkoani Njombe, likidaiwa  kuhusishwa na imani za kishirikina.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Fulgence Ngonyani, alisema
mwanafunzi huyo alikuwa akijaribu kumuokoa mama yake
ambaye alivamiwa nyumbani kwake usiku.

“Watu hao walimjeruhi mwanafunzi huyu kwa mapanga kabla
ya kufanikisha kusudio lake la kutoa msaada na alikufa wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya.

“Awali watu hao walimuua Mwalukolo na baadaye kumfuata
huyu mwanafunzi na kumshambulia, baada ya kipigo alitokwa
na damu nyingi zilizosababisha apotese maisha,” alisema.

Katika tukio jingine, mwili wa mkazi wa kijiji hicho, Estemin Ngogo (80), uliokotwa kwenye korongo lililopo katika Msitu
wa Ikuka Kyambamba, ukiwa umetenganishwa kichwa
na kiwiliwili.

Tukio hilo lilitokea Februari 29 mwaka huu, saa 10 jioni siku
moja tangu marehemu ahusishwe na vitendo vya ushirikina na kutakiwa kuondoka kijijini hapo na yeye kukubali agizo hilo.

Kutokana na makubaliano hayo kati yake na uongozi wa kijiji,
siku iliyofuata aliondoka kwenda kijiji cha jirani ili kufuata fedha ambazo zingemsaidia kuhamisha mali zake ndipo alipokutana na 
wauaji ambao bado hawajafahamika.

Hivi sasa, katika Mkoa huo matukio ya mauaji yamekuwa mengi
na kusababisha hofu kwa wazee ambao wamekuwa wakiuawa
kwa imani za kishirikiana.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Majira, walisema ipo haja ya Serikali kutoa elimu kwa wananchi ili kukomesha vitendo vya mauaji kwa watu wasio na hatia pamoja na viongozi wa vijiji kutumia mikusanyiko ili kutoa elimu hiyo.


1 comment:

  1. Mbona mwaka huu tarehe 29 Februay haikuwepo! Tukio la mwaka huu au la mwaka jana.?

    ReplyDelete