11 March 2013

CCM watoa tamko gesi ya Mtwara



Na Casmir Ndambalilo, Newala

HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara, imeunga mkono tamko la Halmashauri Kuu ya Taifa ya kukubali ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaaam baada ya kubaini wakazi wa Mkoa huo watanufaika na mradi wa gesi uliopo mkoani humo.

Kauli hiyo imetolewa kwa pamoja na wajumbe wa Mkutano wa halmashauri hiyo kwenye kikao kilichofanyika jana katika ukumbi wa shule ya Sekondari ya Kutwa ya Newala mjini chini ya Mwenyekiti wake, Bw. Ali Athumani Sadi.

Wajumbe wa halmashauri hiyo, pia wamekubali kutekeleza pendekezo la Halmashauri ya Taifa CCM ya kushirikiana na
Serikali kuendelea kutoa elimu ya kutosha kwa wakazi wa
Mtwara juu ya mradi wa gesi, rasilimali nyingine za Taifa.

Akifungua katika kikao hicho, Mwenyekiti wa CCM mkoani humo,  Mohamed Sinani, alisema amani na utulivu ndani ya chama hicho ni chachu ya mafanikio ya Serikali kuleta maendeleo ya wananchi.

Alisema makundi ndani ya CCM hayana nafasi wakati huu ambapo kilichobaki ni kushikamana na kutekeleza ilani ya chama kwani kuendelea kudarakana kutawapa nafasi maadui kujipenyeza ili 
kukidhoofisha cham hicho.

“Ipo haja ya kuwa na vikao vya mara kwa mara ili kujadili mikakati ya kuimarisha chama chetu,” alisema.

Akifafanua tamko la Halmashauri Kuu ya Taifa kuhusu mgogoro
wa gesi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Utawala Bora, Kapteni mstaafu, George Mkuchika ambaye pia ni Mbunge
wa Newala, alisema gesi inayopelekwa Dar es Salaam ni asilimia
16 tu ya gesi yote iliyogunduliwa.

Alisema kiasi kinachobaki kitatosheleleza mahitahi ya wakazi wa Mtwara kwa miaka mingi ijayo ambapo ujenzi wa kiwanda cha kusafisha gesi, kitajengwa kwenye Kijiji cha Madimba Mtwara vijijini kama ilivyopangwa.

“Hivi sasa wananchi wa Kata ya Madimba (inakochimbwa gesi), wanaunganishiwa umeme bila malipo na majengo yote yanayotoa huduma kama shule, zahanati, misikiti na makanisa pia tayaunganishiwa,” alisema.

Bw. Mkuchika alisema viwanda vingi vinavyotumia gesi vitajengwa mkoani humo na hakuna kitakachohamishwa ambapo wawekezaji 51 hadi sasa wamejitokeza kuwekeza katika Mkoa huo.

Aliongeza kuwa, ujenzi wa kiwanda kikubwa cha Saruji kuliko vingine Afrika Mashariki na Kati, kinajengwa Mikindani, ambapo jumla ya wafanyakazi 5,000 wataajiriwa na kiwanda cha mbolea kinatarajiwa kujengwa mkoani humo.

Halmashauri Kuu ya Taifa ilipokea maelezo ya Serikali kuhusu maandamano na vurugu zilizotokea mkoani humo Desemba 27,2012 na Januari 25-26 mwaka huu, yakiongozwa na viongozi waliodai kupinga mradi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.



No comments:

Post a Comment