19 March 2013
Chadema :Hatutoki tena Bungeni
Na Suleiman Abeid, Shinyanga
WABUNGE wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wametangaza kubadili utaratibu wao wa kutoka nje ya vikao vya Bunge kutokana na kutoridhishwa na baadhi ya mambo na badala yake sasa watakuwa wakikomaa ndani mpaka kieleweke.
Uamuzi huo umekuja baada ya wabunge hao kukaa chini na kutafakari kwamba tabia ya wao kugomea baadhi ya mambo kwa utaratibu wa kutoka nje ya vikao vya bunge ni sawasawa na mtu kumsusia nguruwe shamba la mihogo ambaye hushambulia mihogo yote na kuimaliza.
Akitangaza uamuzi huo mwishoni mwa wiki iliyopita katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika mjini Shinyanga, Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Sylivester Kasulumbai alisema kuanzia sasa watabadili utaratibu huo na hawatatoka nje pale Bunge linaposhinikiza kupitisha mambo yasiyo na maslahi kwa wananchi.
Kasulumbai alisema CHADEMA imebaini kutokana na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa na wabunge wengi ndani ya bunge mara nyingi wanaamua kutumia mwanya huo kupitisha mambo ya ovyo hata yale ambayo hayana maslahi kwa Watanzania.
Alisema kutokana na hali hiyo wameona ni vyema kuanzia sasa wawe wakitumia nguvu ya hoja katika kutetea masuala mbalimbali bungeni yanayogusa maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha yale yasiyo na maslahi hayapitishwi badala ya utaratibu wa kutoka nje kama ilivyokuwa imezoeleka.
“Wabunge wa CHADEMA sasa tumekubaliana kubadili utaratibu wetu katika kupinga upitishwaji wa hoja zisizo na maslahi kwa wananchi, awali tulikuwa tukisusia na kutoka nje ya Bunge baada ya wenzetu kushinikiza kupitisha hoja hizo, sasa tunasema hatutatoka nje tena,” alisema.
“Tumekaa na kutafakari kwamba hata pale tunapotoka nje, bado kile tulichokuwa tukipinga kisipitishwe wenzetu hukipitisha na kisha wanapongezana, sasa tunasema hatutatoka tena, badala yake tutakomaa humo humo mpaka kieleweke,” alisema Kasulumbai.
Kwa upande wake mwenyekiti wa vijana wa CHADEMA Taifa (BAVICHA), John Heche aliwataka wakazi wa mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu kuchukua hatua za kufanya mabadiliko katika uongozi wa nchi baada ya hali ya maisha inayosababishwa na CCM kuendelea kuwa ngumu kila siku.
Alisema pamoja na sehemu kubwa ya Watanzania kuwa maskini wa kutupwa bado serikali ya CCM imeendelea kuwakumbatia wawekezaji kutoka nje kwa kuwapatia raslimali za nchi huku wenye raslimali hizo wakiendelea kuhangaikia hata mlo wa siku moja na serikali yao ikiomba kusaidiwa vitu ambavyo ina uwezo navyo,"
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment