04 March 2013

JK ashangazwa na matokeo IV *Asema tume ya Pinda itatoa majibu stahiki *Adai vurugu za kidini kamwe hazivumiliki



SAKATA la matokeo mabaya ya wanafunzi waliomaliza kidato
cha nne mwaka 2014, limeigusa Serikali ambayo imekiri kuwa, jamii inahitaji kupatiwa majibu ya uhakika kuhusu anguko hilo.

Rais Jakaya Kikwete, aliyasema hayo juzi katika hotuba anayoitoa kila mwezi kwa wananchi na kusisitiza kuwa, njia pekee ya kubaini chanzo cha anguko hilo ni kuunda tume.

Alisema uchunguzi wa matokeo hayo ni jambo muhimu kwa maendeleo ya nchi ili kuiwezesha Serikali na wadau wengine kuchukua hatua stahiki za kurekebisha tatizo lililopo.

“Serikali imeona umuhimu wa kuunda tume ili kubaini sababu iliyochangia wanafunzi kupata matokeo mabaya kiasi hiki...kama tusipofanya hivyo, mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi na
lawama zitakuwa kubwa kwa Serikali,” alisema.

Aliongeza kuwa, hivi sasa yanatolewa mawazo mengi kuhusu sababu anguko la wanafunzi kwa asilimia 65.5 ambapo wapo
wanaodhani lipo tatizo katika utungaji mitihani, usahihishaji
wake au kutoa maksi kwa watahiniwa. 

Alisema wapo wanaoamini walimu hawawajibiki ipasavyo au
baadhi yao kutokumudu masomo wanayofundisha, wanafunzi
kutokuwa makini masomoni na wazazi kutowajibika kufuatilia
maendeleo ya watoto wao sheleni.

Rais Kikwete alisema, baadhi ya wananchi wanainyooshea
kidole Serikali na kudai sera, mitaala na uwekezaji, haukidhi
mahitaji ya maendeleo ya elimu nchini.

“Wapo wanaofikiria Serikali kushindwa kuongeza mishahara ya walimu kwa asilimia 100 kama walivyotaka pia ni sababu moja
wapo..tumeunda tume hii ili kujua ukweli hivyo naomba kila
mtu awajibike kufikisha mawazo yake ili tupate jawabu
muafala la tatizo hili,” alisema Rais Kikwete.

Aliongeza mwaka 2012, wanafunzi 397,132 walifanya mtihani huo kati yao, waliofaulu 126,851 sawa na asilimia 34.5 na wasiofaulu 240,903 sawa na asilimia 65.5 ambapo matokeo hayo ni mabaya.

Alisema mwaka 2011, wanafunzi 336,782 walifanya mtihani huo kati yao waliofaulu walikuwa asilimia 53.6, wasiofaulu walikuwa asilimia 46.4.  Mwaka 2010, wanafunzi 352,045 walifanya mtihani huo, waliofaulu asilimia 50.4, waliofeli walikuwa asilimia 49.6.

Sakata la Waislamu na Wakristo

Rais Kikwete alisema, kwa miezi kadhaa kumekuwa na matukio  yanayosababisha mifarakano na kupandikiza chuki baina ya waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu. 

Kutokana na hali hiyo, Serikali haitasita kuwachukulia hatua
wote wanaochochea chuki za kidini, wanaodharau vitabu
vitakatifu vya dini nyingine.

“Nimelikumbusha Jeshi la Polisi na mamlaka husika kote nchini, wasifanye ajizi kwenye matukio ya namna hii, wachukue hatua
stahiki kwa wote wanaohusika. 

“Nimewataka wazingatie msemo wa Kiswahili usemao “ajizi nyumba ya njaa”, wachochezi wa mifarakano na chuki za kidini wasipodhibitiwa ipasavyo wataleta maafa kwa Watanzania wasio
na hatia,” alisema Rais Kikwete.

Aliongeza kuwa, Wakuu wa Wilaya na Mikoa kama walinzi
wa amani katika maeneo yao, amewataka watimize wajibu
wao ipasavyo na polisi kukamilisha mapema upelelezi wa
makosa ya vurugu za kidini na wahusika wafikishwe
kwenye vyombo vya sheria iwe fundisho kwa wengine.

Alishangazwa na matukio yanayotokana na imani za kidini
tofauti na miaka ya nyuma kwani Watanzania ni watu wa
kuheshimu tofauti za dini mbalimbali na waelewa ndio
maana wamekuwa wakiishi pamoja kama ndugu.

“Kuna wenzetu kwa sababu wanazozijua wao, wanataka
kuivuruga nchi yetu, tusiwape nafasi wachochezi hawa kwani hawatutakii mema sisi wenyewe na dini zetu,” alisema.

No comments:

Post a Comment