04 March 2013

Siri ya ushindi CCM-2015 yafichuka *Lowassa: Ipo siku Mungu atanipa utajiri



Na Daud Magesa, Mwanza

WAZIRI Mkuu mstaafu, Bw. Edward Lowassa, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitashinda vizuri uchaguzi Mkuu wa 2015, kama Serikali itarejesha utaratibu wa kuwapa mikopo wajasiliamali kupitia ‘Mabilioni ya JK’, ili waweze kujikomboa kiuchumi.

Alisema ili kujiwekea mazingira mazuri ya ushindi wa kishindo katika uchaguzi huo, lazima CCM ione umuhimu wa kurejesha mpango huo ili wananchi waweze kukopeshwa fedha hizo hasa
wanawake waliopo vijijini waweze kukuza kipato chao.

Bw. Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, mkoani Arusha, aliyasema hayo wakati akizindua Mfuko wa Umoja wa Wanawake wa Kikristo jijini Mwanza na Manispaa ya Ilemela, unaofahamika kama Inter Relegance (IR) VICOBA.

“Mimi niliwaambia wanasiasa wenzangu, tukitaka kushinda vizuri uchaguzi mkuu ujao ni vyema tukawasaidia akina mama hasa wa vijijini kwa kuwapa mikopo ili wajikomboe katika umasikini na kujiletea maendeleo,” alisema Bw. Lowassa.

Aliongeza kuwa, yeye ni tajiri wa watu si fedha kinyume na anavyofikiriwa ila anaamini kuwa, ipo siku Mungu atamjalia
na kumpa utajiri kama inavyosemwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Bw. Khamis Mgeja, alisema genge la watu wachache wanaomwandama Bw. Lowassa wakimuhusisha na utajiri, limelenga kumkatisha
tamaa ili asifanye kazi ya Mungu.

“Lowassa si mtu wa dini anayejumuika na watu wa itikadi tofauti, wapo watu wachache wanaotaka kumkatisha tamaa asifanye kazi
ya Mungu...mimi kwa niaba ya wakazi wa Shinyanga, tutafanya maombi ili washindwe na walegee,” alisema Bw. Mgeja.

Bw. Lowassa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, alichangia sh. milioni sita kati ya sh. milioni 40.1 ambazo ni
fedha taslimu zilizochangwa pamoja na ahadi.

Fedha hizo zimevuka lengo la mfuko huo ambalo lilikuwa ni kukusanya sh. milioni 40 ambapo awali, Katibu wa umoja huo
Bi. Paulina Gasabile, alisema wanakabiliwa na changamoto
ya ongezeko la wahitaji.

Umoja huo unahudumia yatima, watu wanaoishi na Virusi vya ugonjwa wa UKIMWI, watoto waishio kwenye mazingira
magumu, wazee pamoja na wajane.

Mfanyabiashara na Mkurugenzi wa Kampuni ya Nyanza Botlling Bw. Christopher Gachuma na mjumbe wa NEC Wilaya ya Tarime, alichangia sh. milioni 8 na mjumbe wa NEC Arumeru Mashariki, Bw. Mathias Manga (sh. milioni 5).

Wengine ni Bw. Vedastus Mathayo na Mkurugenzi wa Gaki Investment ambaye pia ni mjumbe wa NEC Wilaya ya Shinyanga, Bw. Gasper Kileo, walichangia sh. milioni 2 kila mmoja.

Pia Bw. Mgeja, Bw. Raphael Chegeni na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza kila mmoja alichangia sh. 500,000 ambapo Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amina Masenza alichangia sh. 300,000.

No comments:

Post a Comment