05 March 2013

Jela miaka 30 kwa ujangili



Na Mary Margwe, Babati

MAHAKAMA ya Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, imemuhukumu Bw. Hamis Said (32), kutumikia kifungo
cha miaka 30 jela na kulipa faini ya sh. milioni 10.


Bw. Said ambaye ni mkazi wa Singida, anatuhumiwa kukutwa
na bunduki wakati akijiandaa kufanya ujangili wa tembo katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, iliyopo Babati, mkoani humo.

Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mfawidhi wa Wilaya
Bw. Victor Bigambo, ambaye alidai mshtakiwa alikutwa na
kosa hilo Desemba 10,2012, saa 2:35 usiku.

Awali Mwendesha Mashtaka Linus Bugaba, alisema siku ya
tukio mshtakiwa alikutwa na bunduki aina ya Rifle 458, ikiwa
na risasi tano ambayo namba zake zimefutwa.

Alidai mshtakiwa alikuwa amejiandaa kufanya ujangili
wa tembo katika hifadhi hiyo na alikamatwa na askari
wanyamapori waliokuwa kwenye doria.

“Askari wa hidahi hii walifanya doria baada ya kupata taarifa
kutoka kwa raia kuwa mwindaji haramu alionekana akiingia hifadhini akiwa na silaha,” alisema Bugaba.

Alimuomba Hakimu Bigambo atoe adhabu kali mshtakiwa
ili iwe fundisho kwa wengine kwani matukio ya uwindaji
wa wanyamapori nchini yamekithiri.

Hakimu Bigambo alikubaliana na ombi hilo na kutoa hukumu
ya miaka 15 kwa kosa la kukutwa na silaha isivyo halali na lile
la kukutwa na risasi miaka 15.

Alisema mshakiwa atatumikia adhabu hiyo kwa pamoja hivyo atalazimika kukaa gerezani miaka 15.

No comments:

Post a Comment