05 March 2013

Dkt. Bilal: Muungano usidharauliwe


Na Veronica Modest, Butiama

MAKAMU wa Rais Dkt. Mohamed Gharib Bilal, amewataka Watanzania kutoudharau Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar badala yake uheshimiwe na kulindwa.


Alisema Muungano ni kiungo muhimu hivyo jambo la msingi
ni kuhakikisha hauvunjiki ili kuwaenzi waasisi wake Habati
Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.

Dkt. Bilal aliyasema hayo jana wakati akizindua ujenzi wa
barabara ya Nyanguge hadi Musoma, mpakani mwa Mkoa
wa Simiyu na Mara.

Alisema Mkoa wa Mara hauwezi kuenziwa bila kumtaja
Mwalimu Nyerere ambaye katika uongozi wake hakutaka
ubaguzi kati ya Zanzibar na Tanganyika pamoja na
kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali
itikadi za vyama vyao au dini.

“Muungano huu ambao umedumu kwa miaka 50 una umuhimu mkubwa kwa Watanzania hivyo tunapaswa kuudumisha na kuuenzi kwa kuondoa makundi yanyoweza kutubagua,” alisema Dkt. Bilal.

Aliwataka Watanzania kulinda amani iliyopo kwa  kutowapa nafasi watu wabaya wanaotaka kuivunja kwani kama Taifa litaingia katika migogoro, Serikali itashindwa kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na jamii kubwa isiyo na hatia kupoteza maisha.

Aliongeza kuwa, misukosuko inayohatarisha amani ya nchi
inaweza kuharibu sifa ya Tanzania na kusababisha raia wa
mataifa mbalimbali wanaokuja nchini kujifunza jinsi
Watanzania wanavyodumisha amani yao, wataanza
kutucheka na kutuona hatufai.

“Dini isiwe chanzo cha kutuvunjia amani ndani ya nchi yetu,
wajibu wetu kwa kila Mtanzania ni kuwa mlinzi wa nchi yake,
tusipoilinda amani yetu wenyewe, tutachekwa na kuonekana
hatufai...tujitahidi kuondoa ubaguzi wa dini,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Bw. John Tuppa, aliishukuru Serikali kwa kuupatia Mkoa huo miradi mingi ya
ujenzi na ukarabati wa barabara.

Alisema Serikali imejitahidi kutoa fedha kwa wakandarasi ambapo kazi za ukarabati wa barabara mkoani humo imekuwa ikikamilika kwa wakati hivyo kupunguza kero kwa wananchi ambao hufanya shughuli za maendeleo bila kikwazo cha ubovu wa miundombinu.

No comments:

Post a Comment