11 March 2013

INAUZUNISHA*Mwalimu Mkuu ampa mimba mwanafunzi wake *Amefaulu kidato cha kwanza, akwama kuendelea *Mtuhumiwa yupo uraiani,Polisi watupiwa lawama


Na Gift Mongi

MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Kigwe, iliyopo Wilaya
ya Bahi, mkoani Dodoma, Bw. Martin Mbowe, anadaiwa kumpa mimba wanafunzi wake mwenye umri wa miaka 15 (jina tunalo),
hivyo kushindwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza
katika shule ya Serikali mwaka huu.


Akizungumza na gazeti hili, baba mzazi wa mwanafunzi huyo,
Bw. Jeremia Tobay, alisema waligundua mtoto huyo ana mimba mwaka 2012 baada ya kufanya mtihani wa kumaliza darasa la
saba na kuwa nyumbani akisubiri kutangazwa kwa matokeo.

Alisema baada ya matokeo kutangazwa, mwanfunzi huyo alifaulu hivyo alipaswa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kigwe lakini ameshindwa kutokana na ujauzito alionao ambaye amepewa na Bw. Mbowe.

Aliongeza kuwa, baada ya kubaini mwanafunzi huyo alikuwa na ujauzito, alikimbia nyumbani lakini wasamaria walimsaidia kulifikisha jambo hilo polisi.

“Wasamaria walinisaidia kulifikisha jambo hili polisi ila nashangaa mtuhumiwa (Mbowe), hadi sasa yupo nje kwa dhamna na hakuna dalili zozote za kesi yangu kuendelea mbele,” alisema.


Bw. Tobay alisema, uongozi wa Kituo cha Polisi Kigwe, bado haujatoa kipaumbele katika kesi yake badala yake walimtaka
jambo hilo walimalizi nje ya polisi na Bw. Mbowe jambo
ambalo limemsikitisha na kuhisi anahujumiwa.

“Mtuhumiwa (Mbowe), amekuwa akijigamba mtaani kuwa yeye
ni mtumishi wa Serikali na hakuna hatua inayoweza kuchukuliwa dhidi yake bali mimi nimtafute ili tuzungumze si kwenda polisi kama nilivyokuwa nikifanya,” alisema.

Gazeti hili lilifanya jitihada za kumpata Bw. Mbowe ili aweze kuzungumzia tuhuma hizo lakini simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita bila kupokelewa zaidi ya mara 10 na baada ya dakika
chache ilizimwa kabisa.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, David Misime alikiri kuwepo kwa taarifa za tukio hilo katika Kituo cha Polisi Bahi na tayari hatua mbalimbali za kisheria zimeanza kuchukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.

“Ni kweli tukio hili lipo na limeripotiwa katika Kituo cha Polisi
Bahi na jalada lipo kwa wakili wa Serikali anaanda hati ya
mshataka dhidi ya mtuhumiwa na uchunguzi umeshakamilika,” alisema Kamanda Misime.

Aliongeza kuwa, kilichokuwa kinakwamisha kesi hiyo isifikishwe haraka mahakamani ni kubadilika kwa utaratibu ambapo hivi sasa wakili wa Serikali ndiye anayeandaa hati ya mashtaka na kazi hiyo ameshaimaliza tangu jana hivyo mtuhumiwa atafikishwa mahakamani muda wowote.

No comments:

Post a Comment