11 March 2013

Viongozi wa dini walaani wanaohatarisha amaniNa Christina Mokimirya

VIONGOZI wa Jumuiya na Taasisi mbalimbali za kislamu nchini zimeshauri Serikali kuweka utaratibu wa kutambua Jumuiya au Taasisi za kidini kwa nafasi sawa katika uwakilishi wa masuala ya kidini ndani ya serikali.


Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam katika mkutano wa tamko la viongozi wa kislamu juu ya hali ya uvunjifu wa amani na uchochezi wa kidini nchini  Mjumbe wa Baraza la Maulamaa Shekhe Yasin Kachechele alisema kuwa amani ya nchi inatakiwa ilindwe na kila mmoja katika jamii.

Alisema kuwa katika jamii za kidini kunatakiwa kuwe na mahusiano mazuri ili kuleta maelewano miongoni mwa dini mbalimbali hasa waislamu na wakristo.

"Tuepuke kunyosheana kidole na kuelekeza lawama pindi yanapotokea matukio ya kadhaa ya kusikitisha katika jamii kabla ya uchunguzi kufanyika na kujulikana kwa wahusika wa matukio hayo,"alisema.

Alisema tuhuma hizo zinazotolewa kwa upande wa dini moja ndizo zinazopandikiza chuki miongoni mwa jamii moja na nyingine hivyo jamii ielewe kuwa wao ni jamii moja.

Alisema vyombo vya dola vinapaswa kufanya shughuli zake kwa umakini katika kuyafatilia kwa ukaribu matukio hayo ili isiwe chanzo cha kulitumbukiza Taifa katika vurugu za kidini.

"Kwa upande wetu tunaona huu ni wakati muafaka kwa Serikali na jamii mbalimbali kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo yanayojitokeza ili kudumisha amani na utulivu"alisema.

Alisema wanaungana na wapenda amani wote katika kulaani kwa nguvu zote matendo yanayohatarisha kuvunjika kwa amani nchini. 

No comments:

Post a Comment