18 March 2013

IGP Mwema kufungua mkutano wa makachero



Na Frank Geofray, Jeshi la Polisi

WAKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI’s) kutoka Umoja wa Wakuu wa Polisi Kusini mwa Afrika (SARPCCO), leo wanatarajia kuanza mkutano wa siku mbili jijini Dar es Salaam, chini ya Uenyekiti wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa
ya Jinai nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Msemaji wa jeshi hilo nchini, Advera Senso alisema mkutano huo utafunguliwa na Mwenyekiti wa SARPCCO ambaye ni
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema.

Alisema katika mkutano huo, mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo jinsi ya kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa kufanya operesheni za pamoja na ushirikiano kati ya SARPCCO
na Umoja wa Wakuu wa Polisi nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO).

Advera alisema, pia mkutano huo utajadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na wakuu wa polisi wa SARPCCO katika mkutano uliofanyika Zanzibar, Septemba 2012.

“Kamati tendaji za SARPCCO ambazo zinajumuisha wajumbe kutoka nchi wanachama katika nyanja za sheria, mafunzo na kamati tendaji inayoshugulikia mambo ya wanawake na jinsia, zitajadiliana ili kutoka na maazimio ambayo yatapelekwa katika mkutano wa wakuu wa polisi wa SARPCCO, Mei mwaka huu,” alisema.

Katika hatua nyingine, IGP Mwema amesema, wananchi wote wana jukumu la kulinda amani na usalama wa raia badala ya kazi hiyo kuwaachia polisi peke yao.

IGP Mwema aliyasema hayo mwishoni mwa wiki Mji Mpya Mabwepande, wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa
Kituo cha Polisi pamoja na nyumba.

Alisema usalama wa sehemu ya kuishi unaanzishwa na wananchi
waishio sehemu husika na kwamba kituo cha kuzuia wahalifu ni kama hospitali ambapo uhalifu ukitokea, lazima kupatikane majibu ili usiongezeke.

No comments:

Post a Comment