11 March 2013

DC Korogwe amseka ndani Ofisa Misitu

Na Yusuph Mussa, Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga, Bw. Mrisho Gambo, jana alimuamuru Mkuu wa Polisi wilayani humo,
Madaraka Majiga, kumkamata na kumuweka ndani Ofisa
Misitu Wilaya, Bw. Damas Mumwi baada ya kubishana
naye katika Kikao cha Kamati ya Ushauri Wilaya (DCC).

Katika kikao hicho, Bw. Gambo alimweleza Bw. Mumwi juu
ya tuhuma zinazotolewa dhidi yake kuwa anahusika kukata
misitu na baadhi ya wafanyakazi wa Kampuni ya  Mohamed Enterprises ambayo ina mashamba ya Chai Dindira na
Ambangulu kwenye tarafa ya Bungu.

Bw. Gambo aliongeza kuwa, Bw. Mumwi anashirikiana na wafanyakazi wa kampuni hiyo pamoja na baadhi ya watendaji
wa Serikali za vijiji kukata miti kwa kwa ajili ya mbao.

“Kampuni hii inalalamika kuwa wewe (Mumwi), unashirikiana na baadhi ya wafanyakazi wake kuharibu mazingira kwa kukata miti, nimeiagiza kampuni hii iniandikie malalamiko haya kwa maandishi... kwa sasa nakuacha lakini wakiniletea barua
utaona moto wake,” alisema Bw. Gambo.

Hata hivyo, Bw. Mumwi aliamua kujibizana na Bw. Gambo kwa kumwambia, asimtuhumu wakati hana ushahidi wa jambo hilo, ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bw. Sadick Kallaghe, alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Bw. Lucas Mweri, kumuandikia barua ya onyo kwa kubishana na DC.

Kutokana na hali hiyo, Bw. Gambo akaamuru Bw. Mumwi awekwe ndani na asitolewe hadi  watakapojadili kile anachobisha wakati wananchi wametoa taarifa zinazoonesha anavuna misitu.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilayani humo, Bw. Dunstan Mdoe alikunwa
na utendaji kazi wa Bw. Gambo na kusema hatua nyingine
ambazo anapaswa kuzichukua ni kupiga marufuku matumizi
ya misumeno ya mnyororo ambayo ni tishio kwa ukataji miti.

No comments:

Post a Comment