05 March 2013

Bodo Mpya TBS ilete mabadiliko-Dkt. Kigoda


Na Reuben Kagaruki

SERIKALI imeiagiza Bodi ya Mpya ya Shirika la Viwango nchini  (TBS), kufanya haraka mabadiliko ya Menejimenti ya shirika hilo na idara zake ili kukirejesha chombo hicho kwenye hadhi yake.


Mbali na agizo hilo, Memejimenti mpya iliyoteuliwa imepewa
miezi sita kurekebisha kasoro ambazo zimejitokeza na kusababisha utendaji wa TBS kuwa mbaya.

Agizo hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Viwanda
na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda, wakati akizindua Bodi Mpya iliyoteuliwa hivi karibuni kuongoza shirika hilo.

Aliongeza kuwa, kuna makundi ndani ya TBS, hivyo aliitaka Bodi hiyo ihakikishe inayaondoa na kuahidi kuwafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi.

Alisema Serikali imechukua muda mrefu kuteua Bodi hiyo hivyo anaamini itafanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.

“Mmeteuliwa kuisaidia Wizara na kuhakikisha uchumi unawapa walaji kinachostahili hivyo ni lazima msimamie ubora wa viwango kuanzia hatua ya uzalishaji hadi bidhaa inapomfikia mlaji,” alisema.

Aliwata wajumbe wa Bodi hiyo, kuhakikisha kila mmoja anasimamia sheria na kanuni zinazoendesha shirika hilo ili
kuepuka kufanyakazi kwa ubabaishaji.

“Kazi yenu kubwa ni kuisaidia Wizara hasa Waziri kwa masilahi ya Watanzania wote…msifanye maamuzi baadaye yakaleta msuguano, maeneo mnayohudumia ni nyeti na yanawagusa Watanzania hasa kutokana na soko kuvamiwa na kirusi cha bidhaa bandia,” alisema.

Alisema takwimu alizonazo zinaonesha kuwa, asilimia 30 ya bidhaa zilizopo kwenye soko ni feki, bandia au hafifu, hivyo wajumbe wa Bodi wana kazi kubwa ya kuondoa bidhaa hizo.

Alishauri Bodi hiyo kuhakikisha inajenga ushirikiano na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Tume ya Ushindani (TFC), Baraza la Taifa la Kutetea Walaji na Polisi ili kupunguza bidhaa bandia.

Dkt. Kigoda alisema anatambua kuwa TBS inakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa watumishi hawawezi
kufanya kazi peke yao kutokana na ukubwa wa nchini.

Aliongeza kuwa, kuna viwanda bubu katika maeneo mbalimbali na kutolea mfano Kurasini, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam ambavyo vimekuwa vikizalisha bidhaa ambazo hazitumii nembo ya TBS na zinapoingia sokoni Serikali inakosa mapato.

Aliiagiza TBS kuongeza kasi ya kuwapatia nembo wajasiriamali
ili waweze kuongeza soko la bidhaa zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Cuthbert Mhilu, alisema Bodi yake itafanyia kazi haraka maagizo waliyopewa ili kutoa fursa ya utekelezaji wa majukumu mengine.

Aliwataka wajumbe walioteuliwa katika Bodi hiyo kutambua kuwa wana wajibu wa kutumikia shirika, kuepuka kujihusisha na vitendo viovu.

Katika hatua nyingine, bodi hiyo imemteua Bw. Joseph Masikitiko kuwa Kaimu Mkurugenzi wa TBS ambapo kabla ya uteuzi huo, Bw. Masikitiko alikuwa Mkurugenzi wa huduma za shirika.

Bodio hiyo pia ilimteua Leandri Kinabo kuendelea na nafasi yake ya Mkurugenzi wa Utayarishaji Viwango ambapo Bw. Emanuel Itelia aliyekuwa Ofisa Mipango, anakuwa Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za shirika ambapo wote watafanya kazi kwa uangalizi wa miezi sita.

No comments:

Post a Comment