05 March 2013

Rais Kikwete ahimiza ufugaji wa kisasa


Na Freddy Maro, Bagamoyo

RAIS Jakaya Kikwete, amewataka wafugaji nchini kupima na kupanga ardhi kwa ajili ya ufugaji bora wenye tija ili kuepusha
migogoro kati ya wakulima na wafugaji.


Alisema migogoro hiyo inachangiwa na ufugaji wa kuhamahama
ili kutafuta malisho hivyo umefika wakati wa kupima ardhi na kuimiliki kwa ajili ya ufugaji wa kisasa.

Rais Kikwete alitoa wito huo juzi wakati akizungumza na
wafugaji wa Kabila la Wamasai kutoka mikoa ya Pwani na Morogoro ambao walimtembelea nyumbani kwake Kijiji
cha Msoga, Kata ya Chalinze, wilayani Bagamoyo.

“Lazima mtambue kuwa, ufugaji wa kuhamahama hauna tija
kwani hivi sasa, watu wengi wametambua thamani ya ardhi
ambayo wanaipima, kuimiliki hivyo maeneo ya kuchunga
mifugo yanapungua,” alisema Rais Kikwete.

Alisema pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya ufugaji, aliwahimiza wafugaji hao kuotesha majani ili kupata malisho
ya mifugo na kuepuka upungufu wa lishe wakati wa kiangazi.


Awali wafugaji hao wakiongozwa na Laiboni Tikwa Moreto, walimshukuru Rais Kikwete kuwajengea Shule ya Sekondari
kwa ajili ya watoto wao ambayo hivi sasa ina wanafunzi 146.

“Tunakushukuru sana kwa kutujengea Shule ya Sekondari Moreto, hivi sasa watoto wetu wamepata fursa ya kusoma, tuna kuomba utusaidie ili tuweze kuongeza madarasa, mabweni na maji ya kutosha ili wanafunzi waweze kusoma kwa ufanisi,” alisema.

Akijibu ombo hilo, Rais Kikwete aliwapongeza kwa kuitunza
shule hiyo na kusema kuwa, maisha ya kuhamahama kwa wafugaji yanawakosesha watoto wao fursa ya kupata elimu.

Aliahidi kuendelea kuisadia shule hiyo ili watoto wengi zaidi waweze kunufaika na elimu ya sekondari.

Wafugaji hao walipata fursa ya kutembelea shamba la mifugo la Rais Kikwete kijijini kwake Msoga na kujionea ufugaji wa kisasa unaozingatia kanuni bora za kitaalamu ambapo ngo’mbe mmoja anaweza kufikia uzito wa kilo 700.

No comments:

Post a Comment