18 March 2013

Askofu awakemea wanaochoma makanisa


Na Ramadhan Libenanga, Morogoro

ASKOFU wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Morogoro, Telesphor Mkude, amewataka baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa waumini  wa Kiislamu nchini, kuacha kuchoma makanisa kwani kufanya hivyo watavuruga amani na utulivu uliopo.


Alisema huwa anaumia sana anapoona makanisa yakichomwa moto na kuuawa kwa viongozi wa dini bila sababu za msingi jambo ambalo linapaswa kukemewa ili Taifa lisiweze kuingia katika historia mbaya.

Askofu Mkude aliyasema hayo juzi baada ya kumalizika kwa harambee ya ujenzi  kanisa hilo Parokia ya Kigurunyembe, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Jakaya Kikwete.

Aliwataka waumini wa Kikristo kuendelea kuwa watulivu na kumuomba Mungu ili awape moyo wa kuendeleza maombi kwa watu wanofanya vitendo hivyo.

Wakati huo huo, Askofu Mkude alifurahishwa na uteuzi wa Papa mpya Francis I, kutoka nchini Argentina na kuwapongeza Makardnali 115 kwa kufanya uteuzi huo.

Alisema kuwa Papa huyo mwenye miaka 76 ni wa kwanza kutoka Amerika na nje ya Ulaya kwa miaka mingi zaidi ya 400, kwani wengi wao walikuwa wakitokea nchini Italia.

Kwa upande wake, Rais Kikwete aliunga mkono pongezi hizo na kudai kuwa, Papa mpya ni kiongozi anayependa kuwasaidia watu masikini na kusaidia yatima jambo linalofanywa na watu wachache duniani.



No comments:

Post a Comment