11 February 2013

Wawili wa familia moja wafariki dunia

Na Masau Bwire, Tarime

WATOTO wawili wa familia moja walitambuliwa kwa jina moja moja Safina na Tedy
wenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 12 na 13, wanafunzi wa madarasa ya tano
na sita katika shule ya msingi Sabasaba, Tarime mkoani Mara wanadaiwa kufa baada ya
kugongwa na gari wakati wakitoka shuleni.

Ajili hiyo ilitokea jana saa 12.30 jioni eneo Sabasaba, jirani na Kanisa la KKKT
mjini Tarime.

Taarifa zilizopatikana eneo la tukio na kuthibitishwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi
Kanda Maalum ya Tarime Bw. Justus Kamugisha zilisema, ajali hiyo ilitokea baada ya
gari ndogo aina ya Toyota Corola kumshinda dereva na kuacha njia alipokuwa akijaribu
kumkwepa mtembea kwa miguu na kwenda kuwaparamia watoto hao pembeni mwa barabara.

Kati ya watoto hao mmoja alikokotwa na gari hilo na kwenda kumbamiza na kumgandamiza
katika ukuta wa nyumba ya Bw. Stephen Makere ambao ulianguka baada ya kugongwa na
gari hilo na kudaiwa kusababisha kifo cha mtoto huyo papo hapo.

Dereva wa gari hilo alikimbia mara baada ya kutokea kwa ajali hiyo ambapo Kamanda
Kamugisha amemtaka asiwasumbue askari wake kumtafuta bali ajisalimishe mwenyewe
kituo chochote cha polisi.

Hata hivyo Kamanda Kamugisha alisema taarifa rasmi za tukio hilo atazitoa baada ya
kukamilika kwa uchunguzi.

Aidha katika hali isiyo ya kawaida mashuhuda wa ajali hiyo walidai kusikitishwa na
kitendo cha mmiliki wa nyumba iliyogongwa Bw. Makere ambaye walisema, badala ya
kuokoa maisha ya watoto hao waliokuwa wakitapatapa baada ya kugongwa na gari, hasa
aliyekuwa amegandamizwa ukutani, yeye alikuwa akilia kwa kuzunguka gari hilo akisema
ni wapi atapata fedha za kuikarabati nyumba yake.

No comments:

Post a Comment