11 February 2013
Wananchi watakiwa kuacha kuchukua sheria mkononi
Na John Gagarini, Kibaha
SERIKALI imewaonya wananchi wanaojichukulia sheria mkononi kwa kuwaua watuhumiwa badala yake wawapeleke kwenye vyombo husika ili wachukuliwe
hatua za kisheria.
Hayo yalisemwa na kamanda wa polisi mkoani Pwani Ulrich Matei ambaye
alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya sheria (Law Day) na
kusema kuwa watu wengi wamepoteza maisha katika mkoa huo kutokana na watu
kujichukulia sheria mkononi.
Kamanda Matei alisema kuwa vyombo vya kutoa haki vipo hivyo wananchi wa
mkoa huo hawapaswi kuwaua watuhumiwa kwani wengine wanakuwa hawana hatia.
“Watu wengi wameuawa na watu wanaoojiita kuwa wana hasira kali na
kuwafanyia vitendo vya kinyama watuhumiwa wa wizi wa pikipiki, kuku na vitu
vidogovidogo,serikali haitakuwa tayari kuona vitendo hivyo vinaendelea,”
alisema Kamanda Matei.
Alisema kuwa watu hao wanaojiita wenye hasira kali mbali ya kuua watuhumiwa
wameharibu miundombinu mbalimbali ya watu na serikali jambo ambalo ni
kinyume cha sheria.
“Tabia hii kwa sasa imeshamiri na kushika mizizi kwa sasa kwenye mkoa wa
Pwani jambo hili ni kinyume cha sheria na haki za binaadamu kwani hata
katiba inalinda haki ya mtu kuishi,” alisema Kamanda Matei.
Aidha alivitaka vyombo vya kutoa haki kutochelewesha kutoa maamuzi ili
kuondoa dhana kuwa haki haitendeki na kufikia watu kujichukulia sheria
mkononi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment