11 February 2013

Chanzo cha kudondoka majengo



Na Joseph Mwambije,
Songea


SABABU za kuanguka kwa majengo ya siku nyingi katika
Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma zimetajwa katika Kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Songea hivi karibuni kuwa ni kutokana na kutoboa milango
ya maduka katika majengo hayo bila kufuata utaratibu.


Kabla hajasimama Mwenyekiti wa mipango miji Bw. Christian
Matembo kueleza sababu za kuanguka kwa majengo chakavu katika Manispaa hiyo
alisimamama diwani wa Kata ya Ruvuma Bw.Victor Ngongi na kueleza kuwa
kumekuwepo na wimbi la kuanguka majengo ya muda mrefu katika Manispaa hiyo.


Diwani huyo alitoa mfano wa majengo ya muda mrefu yaliyoanguka
kuwa ni jengo moja lililoko katika mtaa wa Delux katikati ya mji wa Songea
na  jingine lililoko katika maeneo ya
Manzese mjini Songea na kuhoji mikakati ya kusimamia majengo hayo yasiendelee
kuanguka na kuwaangukia watu.


Akijibu hoja hizo Mwenyekiti wa Kamati ya mipango miji
katika manispaa ya Songea Bw.  Matembo amesema kuwa wao wenyewe
Madiwani ndio waliosababisha wimbi la kubomoka majengo kwa kuruhusu kutoboa
milango ya biashara  katika majengo  ambayo
yaliyo mengi ni ya muda mrefu.


Alisema kuwa miaka mitano iliyopita Madiwani hao walipitisha
utoboaji wa milango ya biashara kiholela ili wananchi wao wajipatie kipato na
kutoza shilingi 20,000 hivyo uimara wa majengo ulipungua kwa kuwa mengi ni  ya muda
mrefu na kulitaka Baraza hilo
kubadilisha sheria zake ili kunusuru na ubomokaji wa majengo.


Naye Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Bw. Fanuel
Ndemfoo akizungumza kwenye Kikao hicho amesema kuwa tayari wameshaanza
kwaandikia barua ya kubomoa  wamiliki wa
majengo mabovu na  kwamba takwimu za
majengo hayo zinaendelea kuchukuliwa.


Kutokana na wimbi la kubomoka kwa majengo chakavu yaliyoanza
kubomoka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Ruvuma hivi karibuni
Meya wa Manispaa hiyo Bw. Mhagama alitoa siku tano kwa Wamiliki wa majengo
mabovu kuyabomoa kabla Manispaa haijayaboma kwa gharama zao.

1 comment:

  1. Majengo hudondoka kwa sababu ya ukosefu wa umakini katika ujenzi na Teknolojia hafifu.

    ReplyDelete