11 February 2013

Wananchi wakimbilia kwa sangoma kutafuta tiba




IMEBAINIKA kuwa baadhi ya wakazi wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamekuwa wakilazimika kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kutafuta tiba mbadala wakikwepa lugha chafu zinazotolewa na wauguzi katika vituo vya afya vya serikali.


Mbali ya kukwepa lugha chafu za wauguzi hao lakini pia sababu nyingine ni huduma duni zinazotolewa vituoni na wauguzi hao na hivyo wananchi hao kuona ni  bora wakatibiwe kwa waganga wa kienyeji ambako huamini watapata matibabu ya uhakika.

Hali hiyo ilibainishwa mwishoni mwa wiki iliyopita katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu ambapo madiwani walisema vitendo vinavyofanywa na wauguzi hao ni kinyume cha maadili yao ya kazi na vinahatarisha
maisha ya watu.

Walisema tabia ya baadhi ya watu kukimbilia kwa waganga wa kienyeji imechangia ongezeko la vifo vya akinamama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano wilayani humo na hivyo kushauri kuchukuliwa kwa hatua za haraka kuwadhibiti wauguzi
wanaokiuka maadili yao ya kazi.

Wakifafanua madiwani hao walisema katika baadhi ya vituo wauguzi wamekuwa hawafanyi kazi na badala yake kuwaachia kazi zote wafagiaji ambao ndiyo huwahudumia wagonjwa huku wao wenyewe wakiendelea kufanya shughuli zao binafsi.

“Sasa tabia hii kwa kweli inawavunja moyo wananchi hawa wa vijijini ambao mategemeo yao yote ni vituo hivyo vya afya, inasikitisha sana , na ni hatari kwa akinamama wajawazito wanaokuwa na matatizo ya kujifungua wengi wanakerwa na lugha zisizo za
kistaarabu zinazotolewa na wauguzi,”

“Wajawazito kwa kawaida ni watu wa kuangaliwa kwa ukaribu sana hasa pale wanapokuwa na matatizo, sasa wanapokimbilia kwa waganga wa kienyeji ambako hakuna
gari lolote la wagonjwa wanapozidiwa hakuna njia za kuwasaidia hivyo hufariki dunia,” alisema Juke Andrea.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Seke Bugoro, Ferdinand Mpogomi alisema katika kata yake kuna muuguzi ambaye hafanyi kazi na badala yake hupoteza muda mwingi katika masuala ya ulevi hali ambayo kwa muda mrefu imelalamikiwa na wananchi.

Naye mganga mkuu wa wilaya ya Kishapu, Dkt. Daniel Nsaningu alikiri kuwepo kwa vitendo vya baadhi ya wauguzi kutoa lugha chafu kwa wagonjwa na wengine kujihusisha na vitendo vya uombaji rushwa na ulevi.

Dkt. Nsaningu alisema hivi karibuni yeye mwenyewe alimkamata bwana afya mmoja aliyekuwa akipokea rushwa kutoka kwa mgonjwa ambapo kabla ya kumkamata alifanikiwa kumpiga picha wakati akipokea rushwa kutoka kwa mgonjwa.

“Tunajitahidi sana kuwaelekeza hawa watumishi wetu wazingatie maadili yao ya kazi,tuna tatizo moja kubwa la kushindwa kupata ushahidi wa uhakika ili tuwachukulie wahusika hatua za kinidhamu, tunaomba ushirikiano wenu wa karibu katika vita hii ili
kumaliza tatizo hili,” alisema Dkt. Nsaningu.


No comments:

Post a Comment