11 February 2013
Mjumbe NEC amponda mbunge wa CHADEMA
Na Suleiman Abeid,
Meatu
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Mjumbe wa halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) wilayani Meatu, Salum Khamis amewataka wakazi wa jimbo la Meatu kutotegemea tena msaada wa mbunge wao na badala yake wao wenyewe wajikite katika kufanya kazi kwa
bidii ili wajiletee maendeleo.
Khamis alitoa kauli hiyo juzi katika maadhimisho ya miaka 36 ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya kituo kikuu cha mabasi mjini Mwanhuzi ambapo alisema mbunge wa jimbo la Meatu
Meshack Opulukwa ameonesha wazi kutokuwa na uwezo wa kuwatumikia wananchi.
Alisema iwapo wananchi hao wataendelea kukaa wakimtegemea na kumsubiri mbunge huyo awaletee maendeleo aliyokuwa amewaahidi hapo awali basi waelewe wazi kitafika kipindi kingine cha uchaguzi mwaka 2015 wakiwa hawana kitu chochote cha kimaendeleo.
Khamis ambaye aliangushwa na Opulukwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, alisema pamoja na kwamba miradi mingi katika jimbo la Meatu katika kipindi chake ilikuwa imeandaliwa kutekelezwa, lakini jambo la kusikitisha miradi hiyo sasa imesimama kiasi cha wananchi kupigwa na butwaa.
“Ndugu zangu mimi sizungumzi haya kwa uchungu wa kushindwa, hapana kabisa, bali nayasema kwa uchungu nikiwa kama mwana Meatu mwenzenu, katika kipindi changu ninyi wenyewe mliona jinsi tulivyoanza kupiga hatua kubwa katika suala zima la maendeleo,
hasa katika sekta ya elimu, lakini baada ya kuondoka tayari miradi mingi imesimama,”
“Kusimama kwa miradi hii siyo kwamba serikali haina fedha, bali kunatokana na mbunge mliyemchagua kutokuwa na uwezo wa kufuatilia na kusimamia mambo, niliwashangaa kitu gani kiliwavuta hadi mkamchagua, CHADEMA wenyewe hawamwelewi huyu bwana, sisemi
uongo wala simteti, nasikia yupo hapa, na mimi nilimwalika aje,”
“Ukweli mbunge wetu hana uwezo wa kuwatumikia wananchi, naamini hamkumchagua kwa uwezo wake wa kufanya kazi, maana kiuongozi hanishindi hata kidogo, yeye ni bingwa tu wa maneno ya ulaghai, sasa acheni kumtegemea tena chapeni kazi nyinyi wenyewe hadi mwaka 2015, na msikubali kurubuniwa tena na kupoteza kura zenu,” alisema
Khamis.
Huku akishangiliwa na umati wa wana CCM, mjumbe huyo wa NEC alisema mwaka 2015 CCM itahakikisha inawapelekea wakazi wa jimbo la Meatu mgombea mwenye sifa zote akiwa amekamilika na mchapa kazi mzuri ili aweze kusukuma kwa kasi maendeleo katika jimbo hilo.
Wakati huo huo mjumbe huyo wa NEC juzi jioni aliendesha harambee ya Umoja wa vijana
wa CCM (UVCCM) kwa ajili ya kuchangia mashina mawili ya wakereketwa ya Bomani na Mshikamano ambapo kiasi cha shilingi 4,327,400 kilikusanywa, fedha taslimu ikiwa ni shilingi 382,400 na ahadi shilingi 3,945,000.
Khamis mbali ya kuwapongeza vijana wa mashina hayo kwa kuandaa harambee hiyo ili kuwezesha kupata fedha za kuanzishia miradi ya uzalishaji mali itakayowawezesha kujiajiri aliwaomba wawe makini kwa kuhakikisha fedha itakayopatikana inatumika
kwenye malengo yaliyokusudiwa ambapo aliahidi kuwatafutia misaada zaidi kutoka kwa
marafiki zake wengine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment