11 February 2013
Waandishi watakiwa kuwa waadilifu
Rachel Balama na
Rehema Maigala
WAANDISHI wa Habari nchini wametakiwa kuwa waadilifu na kuandika habari za uchunguzi zinazohusiana na rushwa ili ziweze kufanyiwa kazi na kuleta changamoto kwa ajili ya maslahi kwa umma.
Hayo yalisemwa Dar es salaam jana na Mkuu wa sehemu ya Uratibu na Utoaji habari wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini(PCCB) John Kabale wakati akitoa mada katika mkutano wa wadau mbalimbali wa habari ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
"Ni vyema waandishi wa habari kuwa waadilifu kwa kukataa rushwa na badala yake kuandika habari za uchunguzi hususani zile zinazohusu rushwa ili ziweze kufanyiwa kazi kwa maslahi ya Taifa," alisema.
Alisema kuwa waandishi wanapaswa kufanyakazi zao kwa umakini na uadilifu na si kwa kipindi hiki pekee bali hata kwa vipindi vingene vijavyo na wasiogope.
Aliwataka waandishi watumie vizuri nafasi zao kwa kukemea na kuibua mijadala mbalimbali ya rushwa ili kujenga jamii ambayo nayo itakuwa ikipingana na rushwa.
"Waandishi pia wanatakiwa wajisafishe kwanza wao wenyewe katika masuala ya rushwa ili waweze kuwazungumzia jamii kwa ujumla na si kwa mtu binafsi," alisema.
Wakichagia hoja baadhi ya wadau walisema kuwa ili kukabiliana na suala la rushwa ni vyema PCCB kushirikiana vizuri na waandishi wa habari.
Aidha walisema kuwa PCCB isisubiri watu watoe rushwa na kupokea ndipo ianze kufuatilia na badara yake pia iangalie na suala zima la mazingira ya rushwa.
Pia waliongeza kuwa wamiliki wengi wamekuwa na kawaida ya kuanzisha vyombo vya habari kwa maslahi yao binafsi pasipo kuzingangatia sera na sheria zilizowekwa.
Walisema kuwa wapo waandishi na wahariri wanafanyakazi kwenye vyombo vya habari kwa miaka mingi lakini hawajui sera za vyombo wanavyofanyia kazi.
Waliongeza kuwa tatizo la rushwa hata kwa waandishi wa habari halitakwisha iwapo wamiliki wa vyombo hawatajali maslahi ya waandishi wao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment