01 February 2013

TFF yatupa pingamizi zote zilizowekwa



Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ambayo ilikutana Januari 30 mwaka huu imetupa pingamizi zote, zilizowekwa kwa wagombea wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hicho.

Kamati hiyo ilijadili pingamizi zilizowekwa, dhidi ya waombaji uongozi wa TFF na Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPL Board).

Wagombea waliowekewa pingamizi hizo ni Jamal Malinzi na Athuman Nyamlani wanaowania nafasi ya Rais, Michael Wambura (Makamu wa Rais), Yusuf Manji (Mwenyekiti TPL) na Said Mohamed (Makamu Mwenyekiti TPL).

Wengine waliowekewa pingamizi hizo, ambao wanawania nafasi za Ujumbe wa TFF ni Hamad Juma, Ephra Swai, Vedasus Lufano, Eliud Mvela na Athuman Kambi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura kwa niaba ya Katibu Mkuu wa chama hicho Angetile Osiah, ilieleza kwamba pingamizi za Malinzi na Nyamlani zimetupwa kwa kuwa walioweka pingamizi hizo, hawakutokea kutoa utetezi wao.

"Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za TFF, Ibara ya 11(4) katika kikao chake kilichofanyika tarehe 30 Januari 2013, ilijadili pingamizi zilizowekwa dhidi ya waombaji uongozi wa TFF na TPL Board na kutoa maamuzi," ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba Malinzi aliwekewa pingamizi na Agape Fue, huku Nyamlani akipingwa na Mintanga Chacha.

Ilieleza kwamba pingamizi la Wambura, limetupwa kwa kuwa mpingaji mmoja Josea Msengi, hakutokea kutetea pingamizi lake wakati pingamizi alilowekewa na Said Rubeya, halikukidhi matakwa ya kanuni za uchaguzi.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa pingamizi aliyowekewa, Manji na Daniel Kamna na Juma Magoma yametupwa kwa kuwa nayo hayakukidhi matakwa ya uchaguzi.

No comments:

Post a Comment