01 February 2013

Kocha Stars aita wa kuivaa Cameroon *Amir Maftah, John Bocco watemwa



Na Elizabeth Mayemba

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars) inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini kesho kutwa kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimatifa, dhidi ya Cameroon 'Indomitable Lions'.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kim alisema mechi dhidi ya Cameroon itakuwa kipimo kizuri kwake kwa sababu ni sehemu ya maandalizi, kabla ya kucheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco, itakayofanyika Machi mwaka huu.

"Itakuwa mechi ngumu na kipimo kizuri kwetu. Tuko tayari, tutacheza kwa staili yetu kwa sababu ni sehemu ya maandalizi, kabla ya mechi na Morocco. Ni mechi nzuri kwa sababu wachezaji wameonesha wako tayari.

"Tumetoka kucheza dhidi ya Zambia na Ethiopia. Lengo ni Taifa Stars kucheza fainali za AFCON 2015 kwa hiyo, mechi dhidi ya Cameroon ni sehemu ya mipango yetu kuhakikisha tunafika huko," alisema Kim.

Kocha huyo amerejea nchini juzi akitokea Afrika Kusini kuzifuatilia timu za Morocco na Ivory Coast, zilizo kundi moja na Tanzania katika mechi za mchujo za Kombe la Dunia.

Taifa Stars itacheza na Morocco Machi 24 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Stars inashika nafasi ya pili katika kundi lake nyuma ya Ivory Coast, inayoongoza. Timu nyingine katika kundi hilo ni Gambia.

Wachezaji aliowaita kwenye kikosi chake ni makipa Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula (Azam), mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Said 'Cholo' (Simba), Aggrey Morris (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba) na Issa Rashid (Mtibwa Sugar).

Wengine ni viungo ni Amri Kiemba (Simba), Simon Msuva (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Salum Abubakari (Azam), Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd (Yanga) na Mwinyi Kazimoto (Simba).

Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

No comments:

Post a Comment