31 January 2013

Wajasiriamali mnapaswa kungeza nguvu-TIC



Na Mwandishi wetu, Mbeya

KITUO  cha Uwekezaji nchini (TIC) kimesema wajasiriamali nchini wanatakiwa kuongeza nguvu zaidi katika kuendelea biashara kwa kuwa biashara zao ni nguzo ya uchumi wa nchi.


Mratibu wa Mafunzo ya Ujasiriamali wa kituo hicho, Bw.Patrick Chove ambaye pia ni mwezeshaji wa mafunzo ya ujasiriamali alisema hayo mkoani Mbeya kuwa wajasiriamali wana nafasi kubwa ya kuendeleza nchi.

Alisema hayo wakati wa mafunzo ya wajasiriamali katika mkoa huo yaliyotolewa na TIC kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) chini ya  programu ya Business Linkages ya kituo hicho.

“Taifa linatambua mchango wa wajasiriamali ndiyo maana kumekuwa na jitihada nyingi za uwekaji mazingira bora ya biashara,”na kuongeza kusema kuwa ombi kubwa kwao ni kufuata maadili ya kufanya biashara.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa wajasiriamali,TIC inazidi kuendeleza kutoa mafunzo kwa kundi hilo kwa kuwajengea uwezo wa kufanya biashara na wafanyabiashara wa makampuni makubwa.

“Tulianza kutoa mafunzo haya Jijini Dar es Salaam yakaenda Moshi na sasa yameingia Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Mkoa wa Mbeya umekuwa wa kwanza,”alisema Bw.Chove.

Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inajumuisha mikoa ya Ruvuma, Iringa, Rukwa, Katavi na Mbeya yenyewe ambapo ofisi ya kanda ya TIC ndiyo inayoratibu mafunzo hayo katika eneo hilo.

Alieleza kuwa matarajio ya mafunzo hayo ni kuwafikia wajasiriamali wote katika kanda hiyo ili waweze kupata mbinu za biashara na kutoa mchango wao kwa taifa.

Alisema katika mafunzo hayo, wajasiriamali  wanafundishwa tabia za kuwa mfanyabiashara ili waweze kuwa kama wafanyabiashara wengine duniani maana tabia zao zinafanana.

Mshauri kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD), Benedict Lema ambaye pia ni mwezeshaji wa mafunzo ya ujasiriamali alisema kampuni kubwa zinashindwa kufanya biashara na wajasiriamali hapa nchini kwa kuwa baadhi siyo waaminifu.

“Badala ya kununua malighafi za wajasilimali wa hapa, wafanyabiashara wakubwa wanaagiza nje ya nchi,” alisema Bw. Lema, na kuongeza kuwa hali hii haifai kwa maendeleo yao.

Alisema ni muhimu kwa wafanyabiashara wa ndani kujitahidi kuwa waaminifu na kujituma ili kufikia viwango vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment