07 February 2013

Stars yaiduwaza Cameroon *Yaichapa bao 1-0 Taifa



Na Speciroza Joseph

TIMU ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), jana iliwapa uhondo mashabiki wa soka nchini baada ya kuifunga Cameroon 'Simba wasiofugika' bao 1-0, katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Mpira ulianza taratibu, huku kila moja ikiusoma mchezo wa mpinzani wake, lakini dakika ya 26 Erasto Nyoni alikosa bao la mkwaju wa penati, baada ya shuti lake kuokolewa kwa uhodari na kipa, Effala Komguep wa Cameroon.

Penati hiyo ilitolewa na mwamuzi, Munyemana Hudu wa Rwanda baada ya Ngoula kumchezea rafu, Mbwana Samata katika eneo la hatari wakati akienda kufunga.

Lakini kabla ya penati hiyo, dakika ya 25 Cameroon walifanya shambulizi la nguvu langoni mwa Stars, hata hivyo shuti la Aboubakar Vincent likatoka nje ya lango.

Dakika ya 28, Mrisho Ngasa akiwa na lango alikosa bao ambalo liliokolewa na mabeki wa Cameroon.

Cameroon ilijibu shambulizi hilo dakika ya 33 ambapo, Olinga Fabrice aliwachambua mabeki wa Stars lakini shuti lake likadakwa na Kaseja.

Dakika za 38, 40 na 41 washambuliaji wa Stars waliliandama lango la Cameroon, ambapo Mwinyi Kazimoto na Amri Kiemba mashuti yao yalitoka nje na lingine kudakwa na kipa.

Kipindi cha pili Taifa Stars ilifanya mabadiliko kwa kumtoa, Kazimoto na kumwingiza, Thomas Ulimwengu.

Cameroon nayo iliwatoa Tchami Hervena, Edoa Charle na kuwaingiza Eloundu na Olinga Fabrice.

Mabadiliko hayo yaliisaidia zaidi, Stars ambayo ilianza kucheza vyema na kuwabana vilivyo wapinzani wao.

Stars ilipata bao dakika ya 89 lililowekwa kimiani na Mbwana Samata baada ya kuunganisha krosi ya Shomari Kapombe.

Stars: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Kelvin Yondan, Agrey Moris, Salum Abubakari, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Mbwana Samata, Mwinyi Kazimoto na Amri Kiemba.

Cameroon: Effala Komguep, Assou Ekoto, Aminou Bauba, Ngoula, Nyom Allan, Pierre Wome Nlend, Kingue Mpondo, Bedimo Henri, Chami Herve, Olinga Fabrice na Aboubakar Cincent.


No comments:

Post a Comment