07 February 2013

Nigeria yaiadabisha Mali Madiba


DURBAN, Afrika Kusini

Mpira ulianza kwa Nigeria kuikamia mechi hiyo huku ikicheza pasi fupifupi zilizoifanya Mali, kushindwa kuhimili vishindo hivyo.


Dakika ya 16 Mali waliokuwa wakiongozwa na mshambuliaji, Saydou Keita aliyewahi kuichezea Barcelona nusura wangepata bao lakini shuti la mshambuliaji wake likapaa nje ya lango.

Nigeria baada ya hapo ilianza kuliandama lango la Mali ambapo dakika ya 24, Victor Moses aliichambua lango la wapinzani wao na kuachia mpira wa krosi safi iliyomkuta Ekeje aliyeruka kwa chini na kupachika bao kwa kichwa.

Baada ya bao hilo Nigeria iliendelea kuinyanyasa Mali ambapo dakika ya 29, Moses alifanya kazi nzuri kwa kupiga krosi nzuri iliyomkuta Aide Edeye ambaye hakufanya makosa baada ya kuutumbukiza mpira kimiani na kuwa bao la pili.

Mali nayo ambayo washambuliaji wake hasa, Keita kwa kubanwa na wachezaji watatu wa Nigeria kitu kilichowafanya Thai hao kukosa mbinu za kufunga bao na kujikuta wakipiga mipira iliyotoka nje ama kuokolewa kuwa kona.

Dakika 44 Emmanuel Eminike, ambaye alikuwa akishirikiana vyema na Moses aliifungia Nigeria bao la tatu kwa mkwaju wa faulo, ambayo kabla ya kutolewa mchezaji huyo alifanyiwa madhambi eneo la hatari.

Kipindi cha pili Mali, ilijaribu kujikakamua kwa kuingia kwa nguvu ambapo Keydou akiwa na kipa Vicent Enyiama wa Nigeria aliachia shuti kali ambalo hata hivyo lilitoka nje ya mwamba.

Hata hivyo Nigeria walijipanga vyema na kuendelea kuinyanyasa Mali, kwani dakika ya 59 Ahmed Mousa aliyeingia badala ya Moses, aliiongezea timu yake bao la nne kwa kumpiga toba kipa wa Mali.

Dakika 71 kipa, Enyiama alifanya kazi nzuri baada ya Mali kufanya shambulizi la nguvu ambapo Mamadou Traore aliyeachia shuti kali liliokolewa kwa ustadi na kipa huyo mkongwe.

Juhudi za Mali zilizaa matunda dakika ya 75 baada ya mshambuliaji Adam Tamraura, kumchambua Enyiama na kuipatia timu yake bao la kufutia machozi.



No comments:

Post a Comment