08 February 2013

Serikali yaahidi kulipa malipo ya sensa kwa watendaji


Rose Itono na Peter Mwenda

SERIKALI imetoa ahadi ya kuwalipa Wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa ambao hawajalipwa fedha zao katika mchakato wa Sensa ya Watu na Makazi kabla mwaka huu haujaisha.


Nabu Waziri wa Fedha, Bi. Saada Salum, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu , Bi. Bernadetha Kasabago (CCM).

Bi. Salum alidai kuwa, Serikali imeshafanya uchambuzi yakinifu ili kuwabaini watu wanaostahili kulipwa na tayari imetenga sh. bilioni 4. 2 kwa ajili ya malipo hayo.

Alisema malipo yaliyopaswa kulipwa kwa siku ni sh 10,000 badala ya sh 2,500 walizolipwa na kuongeza kuwa, hali hiyo imetokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza na kusababisha Wenyeviti wa vijiji na vitongoji, kulipwa fedha hizo katika siku saba za kazi hiyo.

“Sh. 2,500 walizokuwa wakilipwa Watendaji na Wenyeviti wa Mitaa, vijiji na votongoji ni kutokana na Serikali kutotenga fedha
kwa ajili yao,” alisema Bi. Salum.

Mbunge wa Viti Maalumu, mkoani Singida, Bi. Martha Mlata (CCM), alitaka kujua kwanini bajeti za Ulinzi na Usalama hazisomwi hadharani, je, kwanini Waziri asiende kujifunza
katika nchi za China, Marekani na India.

Alisema mkoani Singida, askari polisi wanaishi katika nyumba zinazofanana na stoo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Bw. Pereira Silima, alisema ulinzi ni jambo muhimu ili mambo
mengine yaweze kufanikiwa lakini Tanzania inakwenda hatua kwa hatua ila haijafikia kiweango cha kuwa na askari wa kutosha.

Akizungumzia suala la kuwa na nyumba za kutosha za askari,
Bw. Silima alisema Serikali inalifahamu tatizo lililopo na inafanya jitihada za kuhakikisha wanapata nyumba bora hatua kwa hatua.

Mbunge wa Ubungo, Bw. John Mnyika, aliuliza ukiuondoa siri za jeshi ambazo ni nyeti, kwanini Serikali imekuwa na kawaida ya kuficha mapato, matumizi na ufisadi unaofanywa na kampuni
zilizopo chini ya jeshi kama Meremeta.

Akijibu swali hilo, Bw. Silima alisema Serikali imekuwa wazi katika mambo mbalimbali na kudai kuwa, hesabu za kampuni hizo ziko wazi na zinaweza kukaguliwa akitolea mfano kesi zilizofunguliwa mahakamani zikiwahusu baadhi ya Maofisa wa JKT.

No comments:

Post a Comment