08 February 2013
UZINDUZI VITAMBULISHO VYA TAIFA Kikwete awaonya watendaji NIDA *Asema wasiostahili kupata vitambulisho wasipewe *Adai hatawavumilia watakaokiuka maadili ya kazi
Na Mariam Mziwanda
KITENDAWILI cha upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa, kimeteguliwa Dar es Salaam jana na Rais Jakaya Kikwete,
baada ya kuzindua Mfumo wa Taifa wa Usajili, Utambuzi
wa Watu na Utoaji wa vitambulisho hivyo.
Uzinduzi huo umefanyika katika Viwanja vya Karimjee
ambapo mchakato huo, unaratibiwa na Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Katika uzinduzi huo, Rais Kikwete aliwataka watendaji wanaofanikisha utoaji wa vitambulisho hivyo, kuwa
waadilifu na waaminifu katika kutekeleza kazi zao.
Alisema hali hiyo itaepusha utoaji vitambulisho usiostahili na kusisitiza kuwa, hatasita kumchukulia hatua mtendaji yeyote ambaye itabainika amekwenda kinyume na maadili ya kazi hiyo ili kuepuka makosa yanayoendelea kujitokeza katika utoaji wa hati za kusafiria (passport), ambazo zinaligharimu Taifa.
“Watendaji mnadhamana kubwa kwa Taifa, sitakua na huruma kwa mtendaji yeyote ambaye atafanya mchezo mchafu katika mchakato huu kwa kuwapatia vitambulisho vya urai watu wasiostahili, tatizo hili lipo katika utoaji wa hati za kusafiria,” alisema.
Aliongeza kuwa ni vyema Mamlaka na Wizara kuchukua tahadhari mapema ili kudhibiti vitendo vya udanganyifu ambavyo vilianza kujitokeza awali hasa jijini Dar es Salaam.
Alimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, kutokuwa na msamaha kwa watu wote waliohusika
kutoa taarifa za uongo na uuzaji wa fomu.
“Tumepita mabonde na milima, baadhi ya viongozi tulikua tukikosana kwa sababu ya vitambulisho hivi, nchi mbalimbali
duniani zinatekeleza mpango huu mbali ya gharama zake
kuwa kubwa,” alisema Rais Kikwete.
Aliwahimiza Watanzania kuwa wazalendo na walinzi kwa
kuzudisha ushirikiano wa kuwatambua wakazi wanaostahili
kuvipata vitambulisho hivyo vyenye umuhimu mkubwa.
“Serikali itagharamia mchakato mzima wa kupata vitambulisho
hivi ili kuondoa changamoto zilizojitokeza awali...Wizara ya Fedha itenge fungu la kutosha kwa masilahi ya Taifa,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa NIDA, Bw. Dickson Maimu, alisema utoaji wa vitambulisho hivyo ni mpango wa Serikali kuwatambua wananchi wake ili iweze kuwahudumia kwa
wakati na kusisitiza kuwa, utoaji huo utaendelea kufanyika
kwa awamu hadi kuwafikia wananchi wote.
“Umuhimu wa vitambulisho hivi kwa Taifa ni mkubwa hasa katika ukusanyaji kodi, utambuzi wa kiuchumi, kiraia na kiusalama hivyo Serikali inawajibu wa kutatua changamoto zilizopo ikiwemo upatikanaji fedha za mahitaji na rasilimali watu,” alisema
Naye Dkt. Nchimbi alisema mfumo huo ambao mchakato wake ulianza Julai mosi 2008, umekamilika lakini kuna tatizo la baadhi
ya waombaji, kutumia njia zisizo sahihi kutaka kupata
vitambulisho hivyo wakati hastahili.
Makundi mbalimbali yakiongozwa na Rais Kikwete walipatiwa vitambulisho vya awali na kati yao, alikuwepo Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa
Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa.
Wengine ni Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Shariff
Hamad, kada wa CCM Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Dkt. Alex Malasusa.
Pia Rais Kikwete alikabidhi kitambulisho kwa Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, Mwenyekiti wa
CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika
la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Dkt. Ramadhani Dau na Mkurugenzi
Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma Bw.
William Erio.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment