18 February 2013

Serikali iongeze mishahara kwa watumishi-CCM


Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeitaka Serikali iongeze mishahara ya watumishi wake ili waweze kutekeleza majukumu
yao kwa ufanisi mkubwa na kukidhi mahitaji ya sasa.


Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Bw. Nape Nnauye, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akihutubia mamia ya wananchi wa Jimbo la Ubungo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Goba, wilayani Kinondoni.

Alisema baadhi ya makundi katika utumishi wa umma, yapo nyuma kimaendeleo kitokana na kiwango kidogo cha mshshara ambacho wanakipata kutokidhi mahitaji yao.

“Makundi haya ni pamoja na walimu, wahudumu wa vituo
vya afya na watendaji wa kada za chini, wapewe kipaumbele
kwa kupandishiwa mishahara yao.

“Ndugu zangu, hakuna asiyejua umuhimu wa walimu na wahudumu wa sekta ya afya ambao kama watalipwa vizuri, itakuwa motisha kwao ya kutekeleza majukumu yao kwa tija zaid hivyo ni lazima serikali itoe kipaumbele maalumu kwao,” alisema Bw. Nnauye.

Alisisitiza kuwa, Serikali imekuwa ikiongeza mishahara ya watumishi wa umma lakini kutokana na mazingira ya sasa, kiwango ambacho kimekuwa kikiongezwa bado hakikidhi changamoto za maisha ya sasa ambayo kila kitu kinahitaji fedha ili kukipata.

“Miaka iliyopita, mtu alikuwa anaweza kuwa na fedha kidogo sana lakini akafanya mambo mengi mazuri tofauti na sasa, bila pesa hakuna linalowezekana hivyo ni muhimu kuwaongeza mshahara watumishi wa umma ili wawajibike vizuri,” alisema.

Wakati huo huo, Bw. Nnauye aliwataka wapinzani kuacha tabia
ya kupinga kila jambo linalosemwa au kufanywa na Serikali ya
CCM kwa kisingizio cha upinzani badala yake linapotokea suala
lenye masilahi kwa umma ni vyema wakawa kitu kimoja.

Aliwashangaa wanasiasa wanaotumia muda mwingi kubeza mafanikio yaliyoletwa na Serikali ya CCM na kusisitiza kuwa
tabia hiyo ikiota mizizi italeta madhara makubwa.

No comments:

Post a Comment