27 February 2013

Serikali imetimiza ndoto yangu Bumbuli-Makamba


Na Yusuph Mussa, Lushoto

KATIBU Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Bw. Yusufu Makamba, amesema Serikali imeweza kutimiza ndoto yake baada ya Jimbo la Bumbuli kuwa halmashauri kamili.


Alisema furaha nyingine aliyonayo ni kuona mtoto wake Bw. January Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni mbunge wa Bumbuli wa
jimbo hilo, akilithi 'mikoba' kwenye chama na Serikali.

Mzee Makamba aliyasema hayo juzi katika sherehe za uzinduzi
wa halmashauri hiyo zilizofanyika kwenye Uwanja wa mpira Bumbuli na kuongeza kuwa, kama leo hii atondoka duniani
kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, roho yake iko radhi.

“Kulikuwa na mzee mmoja anaitwa Simioni ambaye alimuomba Mungu asimchukue kabla hajamuona mwokozi wa Ulimwengu
Yesu Kristo ambaye sita baada ya kuzaliwa, alikwenda kumuona
na kumwambia Mungu, tayari nimemuona hivyo nichukue.

“Na mimi kwa kuiona Bumbuli inakuwa halmashauri na January anakuwa kiongozi, basi Mungu nipo tayari anichukue, sijui wenzangu akina Shekimweri (aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa), Shempemba na Magogo (wabunge wa Lushoto),” alisema.

Aliongeza kuwa, maendeleo hayaletwi na Serikali bali wananchi wenyewe kwa kushiriki shughuli za msalagambo na kuwataka  viongozi wa vijiji, kata na halmashauri walinde fedha za wananchi badaola ya kuziweka katika mifuko yao ili kiama kisiwakute.

Kwa upande wake, mbunge wa jimbo hilo Bw. Makamba alisema kuwepo kwa halmashauri hiyo, kutaharakisha shughuli za maendeleo ya wananchi.

Alisema tatizo la maji kwenye mji huo na baadhi ya kata litakwisha Juni mwaka huu na kuwataka wananchi wasikate tamaa kuchangia maendeleo ya elimu nchini kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne lakini Serikali inafanya jitihada za kulipatia ufumbuzi.

Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Dkt. Henry Shekifu, alisema tusiweke reheni amani ya nchi kwa kuingiza udini, ukabila na ukanda katika suala la maendeleo.

“Maendeleo tunayoyaona yametokana na amani tuliyonayo pamoja na utulivu, ikitoweka wananchi hawataweza kufanya lolote zaidi ya kuponya maisha yao,” alisema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bw. Amir Shehiza aliahidi kulinda rasilimali zote za wananchi pamoja na kudhibiti 'mchwa' wa halmashauri.

No comments:

Post a Comment