27 February 2013

Mramba: Rais alipendekeza ukaguzi wa migodi


Na Rehema Mohamed

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Bw. Basil Mramba, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa, mazungumzo juu ya ukaguzi wa migodi ya dhahabu, yalianza baada ya Rais kutoa kibali.


Bw. Mramba alieleza hayo mahakamani hapo jana wakati akiendelea kutoa utetezi wake mbele ya jopo la mahakimu watatu wanaosikiliza kesi hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti Jaji John Utamwa.

Alidai mazungumzo hayo yalihusisha Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Wizara ya Fedha
na Wizara ya Nishati na Madini.

Aliongeza kuwa, Mei 11,2003, Rais aliandika barua iliyohusu pendekezo lake kuhusu umuhimu wa kuanzishwa ukaguzi
wa migodi ya dhahabu nchini.

Alidai taratibu za kushughulikia malipo ya gharama za ukaguzi wa madini, zilianza kabla ya makubaliano ya mkataba wa kufanya kazi hiyo kati ya Kampuni ya Alex Stuwart na Serikali haujasainiwa.

Alisema alitoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo bila kulitaarifu Baraza la Mawaziri ambapo mkataba huo aliupeleka katika baraza hilo mwaka 2004.

“Sigfahamu kama makubaliano ya mkataba yalifanyika Mei 23,2003 na kama kulikuwa na muda maalumu wa kusaini mkataba huu baada ya kufikia makubaliano,” alisema.

Alidai moja ya vigezo vilivyotumika kuisamehe kodi kampuni hiyo ni kuangalia masilahi ya umma ili kujua kiasi cha dhahabu ambacho kinazalishwa nchini na kile kinachoibwa.

Katika kesi hiyo Bw. Mramba na wenzake wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 11.7.

Washtakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Bw. Daniel Yona na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Mipango na Uchumi, Bw. Gray Mgonja.

No comments:

Post a Comment