27 February 2013

Pinda: Hatukukosea kuunda tume *Asema lengo ni kubaini kiini cha tatizoRachel Balama na Anneth Kagenda

WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amesema tume iliyoiunda ili kuchunguza matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa Februari 18 mwaka huu, itaanza kazi siku mbili au tatu zijazo.


Bw. Pinda aliyasema hayo Dar es salaam jana wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua ni lini
tume hiyo itaanza kazi na kuongeza kuwa, pamoja na watu
kuipinga, Serikali haikukosea kuiunda ili ifanye uchunguzi
wa kina kubaini kiini cha tatizo.

“Yanayosemwa ni mengi...wapo wanaosema tatizo linajulikana, jambo ambalo si kweli hivyo lazima tume ichunguze ili kujua mkweli na muongo,” alisema Bw. Pinda.

Aliongeza kuwa, tume hiyo pia itachunguza maeneo mengine
yenye utata mkubwa ili kuona jambo hilo halitokei tena.

Hivi karibuni, Bw. Pinda aliunda tume itakayochunguza sababu
ya matokeo mabaya kwa wanafunzi wengi waliofanya mtihani
wa kidato cha nne mwaka 2012.

Asilimia 60 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo walipata sifuri ambapo tume hiyo itajumuisha Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi, Chama cha Walimu nchini (CWT), Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari nchini (Tahossa).

No comments:

Post a Comment